Wasomali kilimo ndio muarobaini wenu

28 Machi 2018

Kilimo, ufugaji na uvuvi sasa ndio mwelekeo Somalia, kazi kwa serikali na wadau kuhakikisha hilo linawezekana.

Kilimo kinasalia kuwa uti wa mgongo wa kuinua uchumi wa Somalia na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Dunia na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, ripoti iliyoweka bayana changamoto zinazopaswa kushughulikiwa ili fursa ziweze kupatikana na kufanikisha suala hilo.

Changamoto hizo ni ukosefu wa usalama kwa zaidi ya miongo mitatu, hali mbaya ya hewa iliyochochea ukame na mafuriko pamoja na ukosefu wa utawala bora.

Ripoti inasema mambo hayo yamesababisha kilimo kudorora kwenye kusini-kati mwa Somalia, halikadhalika sekta ya uvuvi na ufugaji.

Pascal Sanginga, ambaye ni Afisa mwandamizi wa FAO kitengo cha uwekezaji amesema hata hivyo kwa sasa ongezeko la vyakula vinavyogaziwa kutoka nje ya Somalia ni kiashiria cha ongezeko la mahitaji na hivyo kudokeza kuwa ni fursa kwa wafanyabiashara kuwekeza kwenye kilimo cha kibiashara.

Amesema kinachohitajka ni serikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wasomali waishio ughaibuni waweze kushiriki na hivyo hatimaye kupunguza njaa na umaskini.

Kwa sasa mazao kama vile ufuta, malimao yaliyokaushwa ni miongoni mwa bidhaa zinazoongoza kwa kuuzwa nje ya nchi ya Somalia na hii ni baada ya kuporomoka kwa uwezo wa nchi hiyo kuuza ndizi nchi za nje.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter