Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudi yaahidi dola milioni 930 kuwanusuru Wayemen:

Katibu Mkuu Antonio Guterres amekutana na Mwana mfalme wa Saudia Mohammed bin Salman Al Saud,
Picha na UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu Antonio Guterres amekutana na Mwana mfalme wa Saudia Mohammed bin Salman Al Saud,

Saudi yaahidi dola milioni 930 kuwanusuru Wayemen:

Amani na Usalama

Ufalme wa Saudia umeahidi kutoa dola milioni 930 kwa ajili ya mfuko wa usaidizi wa kibinadamu kwa watu wa Yemen.

Ahadi hiyo imewasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo alipokutana na mwana mfalme Mohammad Bin Salman Al Saudi, ambaye pia ni naibu waziri mkuu na waziri wa ulinzi wa ufalme huo.

Katika mkutano wao kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani, Katibu Mkuu amemshukuru Prince Mohammad na ufalme mzima wa Saudia kwa msaada huo mkubwa na moyo wa kujitolea  na kuongeza kuwa fedha hizo zitaziba pengo la theluthi moja ya fedha zote zinazohitajika kwa kukidhi mahitaji ya kibinadamu Yemen mwaka 2018 ambazo ni dola bilioni 2.96.

Msaada huo utauwezesha Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu kupunguza madhila kwa watu zaidi ya milioni 22 wanaohitaji msaada wa kibinadamu Yemen wakiwemo watu milioni 2 ambao ni wakaimbizi wa ndani.

Image
Mvulana mdogo anaendesha tai yake karibu na jengo lililoharibiwa na mikombora huko Saada Yemen. File: OCHA / G.Clarke

Hata hivyo Guterres amesema pamoja na msaada huo uliotolewa na Saudia bado kuna pengo kubwa la dola bilioni 2 kusaidia mgogoro wa kibinadamu Yemen ambao ni mbaya zaidi duniani.

Ili kuhakikisha fedha zaidi zinapatikana kunusuru maisha ya mamilioni ya watu wa Yemen , Umoja wa Mataifa utafanya tukio maalumu la harambee mjini Geneva Uswis Aprili 3.

Pia mwana mfalme huyo na Katibu Mkuu wamejadili wajibu wa kila mmoja katika mgogoro wa Yemen hasa kushirikiana kupata suluhu ya kisiasa kupitia mjadiliano yanayojumuisha pande zote, na  Guterres amesisitiza kuwa kumaliza vita ndio njia pekee ya kumazila zahma ya kibinadamu Yemen.

TAGS: Yemen, Antonio Guterres, Saudi Arabia.