Skip to main content

Eh Mungu geuzia uso wako kwa wana Sudan Kusini- Mkimbizi

Amani ya kudumu nchini Sudan Kusini ni muarobaini kwa mustakhbali wa watoto kama hawa nchini humo ambao sasa haki zao za msingi zinasiginwa.
UNMISS
Amani ya kudumu nchini Sudan Kusini ni muarobaini kwa mustakhbali wa watoto kama hawa nchini humo ambao sasa haki zao za msingi zinasiginwa.

Eh Mungu geuzia uso wako kwa wana Sudan Kusini- Mkimbizi

Amani na Usalama

Tangu mwezi disemba mwaka 2013, Sudan K usini imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Maelfu ya watu wamekimbilia nchi jirani na wengine wamesaka hifadhi kwenye maeneo mengine ya nchi. Hata hivyo hivi sasa wengine wameamua kurejea na kilio chao sasa ni kwa mwenyezi Mungu.

Nchini Sudan Kusini msimu wa mvua ukitarajiwa kuanza, baadhi ya wakimbizi wa ndani na hata wale waliokimbilia nchi za jirani wameamua kurudi nyumbani angalau kuendelea na maisha yao. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Nats..

Hapa ni Kajo Keji, mji ulioko jimbo la Equitoria ya Kati nchini Sudan Kusini. Eneo hilo lilikuwa mahame tangu kuanza kwa mzozo nchini humo mwezi disemba mwaka 2013.

Nats..

Hivi sasa nuru ya amani imewezesha baadhi ya wakimbizi kurejea ili kuendeleza maisha yao na miongoni mwao ni Grace Kobong akikagua lililokuwa shamba lake la mihogo.

(Sauti ya Grace Kobong)

“Napanga kurejea hapa na kuishi. Mwanangu alifariki dunia na sina mtu wa kunisaidia. Alizoea kuja na kunisaidia kuvuna mihogo lakini sasa hayupo. Nimerejea ili nilime na nasaka mbegu za mahindi nipande.”

Tume ya usaidizi na urekebishaji Sudan Kusini iliandaa semina kujadili jinsi ya kusaidia wakimbizi wanaorejea na kusihi jamii ya kimataifa isaidie kwa hali na mali ili hata wakulima waweze kufanya shughuli zao na hivyo kupata chakula.

Grace ana matumaini.

(Sauti ya Grace Kobong)

 “Nina Imani, ninasali ili amani irejee nchini mwetu. Ninaomba ili Mungu atugeuzie uso wake. Hebu na amani irejee kwenye nchi hii.”