Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea Uturuki: Zeid

20 Machi 2018

Ripoti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imebaini kwamba hali ya dharura iliyotangazwa kwa mfululizo na mamlaka nchini Uturuki imesababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya  maelfu ya raia nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayojumuisha matukio ya tarehe mosi Januari  hadi Disemba 2017, baada ya jaribio la kumpindua rais Recep Tayyip Erdoğan  hapo tarehe 15 Julai mwaka 2016, imesababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, mmomonyoko wa utawala wa sheria nchini Uturuki, na huenda ikaathiri hali ya kiuchumi  siku za usoni.

Bwana  Zeid Ra’ad Al Hussein mkuu wa ofisi ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hadi sasa zaidi ya watu 160,000 wametiwa nguvuni , watumishi wa umma laki moja na nusu ikiwemo, walimu, majaji na wanasheria wamefukuzwa kazi ndani ya miezi 18 tu, huku zaidi ya waandishi wa  wahabari 300 na wanaharati wa haki za binadamu kutiwa mbaroni bila kufuata taratibu za kisheria kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

Ripoti hiyo imekusanywa  kutokana na  ushahidi wa ndugu wa  wahanga waliofanikiwa kutoroka ,uchambuzi wa habari za Serikali, nyaraka za vyanzo huru ,  picha za satelaiti na  pia vyanzo vingine vinavyoaminika .

Ofisi ya haki za binadamu imetoa wito kwa serikali ya Uturuki kuruhusu Ofisi ya haki za binadamu kufanya uchunguzi kamili,  kufanya kazi kwa uhuru na kwa kujitegemea ili iweze kufanya  tathmini sahihi ya  hali ya haki za binadamu Kusini-Mashariki mwa nchi hiyo.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter