Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia kumechachamaa, 10,000 waomba hifadhi Kenya: UNHCR

Wahamiaji kutoka Ethiopia. Picha ya IOM/T. Craig Murphy, 2016

Ethiopia kumechachamaa, 10,000 waomba hifadhi Kenya: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Takriban raia 10,000 wa Ethiopia wamewasili nchini Kenya na kuomba hifadhi kufuatia machafuko yanayoendelea nchini mwao.

Hayo ni kwa mujibu wa shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ambalo limekuwa msitari wa mbele kuhakikisha wanapowasili katika eneo la Moyale wanapatiwa huduma muhimu ikiwemo chakula na malazi.

Wakimbizi hao wamekuwa wakisimulia madhalia waliyopitia huku wengine wakilazimika kutembea siku kadhaa bila kula wala kunywa, na pia kushuhudia ukatili wa kutisha wakati jeshi la Ethiopia liliposhambulia vijiji katika maeneo ya upinzani.

UNHCR inasema kwa kipindi cha wiki iliyopita pekee wakimbizi 9,700 waliwasili Moyale wakitokea jimbo la Oromia nchini Ethiopia na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Balanish Tadese, mmoja  kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya
UNHCR/Rose Ogola
Balanish Tadese, mmoja kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya

Limeongeza kuwa miongoni mwa waoomba hifadhi hao 600 ni kina mama wajawazito, watoto karibu 1500 wa umri wa chini ya miaka 5, na wengine ni walemavu na wazee.

Watu hao ambao kwa sasa wanaishi katika makambi mawili ya Somare na Sololo Moyale, na wanahitaji msaada wa haraka wa chakula, maji, vifaa vya usafi na kujisafi, malazi na huduma za afya.

UNHCR inaongoza na kuratibu misaada kwa ajili yao na imeaanza kuwagawia mablanketi, sabuni, madumu ya maji, vyombo vya kupikia, vyandarua vya mbu na magodoro.