Wakimbizi Warohingya wako katika hatihati bila dola milioni 951: UN

Wanawake na watoto wasubiri msaada wa kibinadamu Cox's Bazar, Bangladesh, ambapo milioni moja ya wakimbizi wa Rohingya wamehifadhiwa.
Olivia Headon/IOM
Wanawake na watoto wasubiri msaada wa kibinadamu Cox's Bazar, Bangladesh, ambapo milioni moja ya wakimbizi wa Rohingya wamehifadhiwa.

Wakimbizi Warohingya wako katika hatihati bila dola milioni 951: UN

Msaada wa Kibinadamu

Mpango wa pamoja wa kunusuru maelfu ya wakimbizi wa Rohingya kutokana na janga la kibinadamu, umezinduliwa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswis , ukihitaji dola zaidi ya milioni 900.

Mpango huo ujulikanao kama JRP umezinduliwa na Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi, UNHCR bwana Filippo Grandi, mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, William Lacy Swing na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bangladesh Bi Mia Seppo.

Wakizindua mpango huo mjini Geneva maafisa hao wa Umoja wamtaifa wameomba dola milioni 951 kwaajili ya msaada utakaokidhi mahitaji ya kuanzia sasa hadi Desemba 2018 ya watu milioni 1.3, wakiwemo wakimbizi wa Rohingya 884, 000 na watu 336,000 wa jamii zinazowahifadhi.

Image
Wakimbizi wa Rohingya wapatiwa huduma za afya kambini Kutopalong. Picha: UNHCR

Mkuu wa UNHCR Filipo Grandi akisisitiza hilo amesema

(SAUTI YA FILIPO GRANDI)

“Ombi linajikita na hali ya wakimbizi kwa sababu hilo ndilo tunalotaka kuisaidia serikali ya Bangladesh na hali ni mbaya sana, tunaisaidia Bangladesh lakini tunahitaji ffedha zaidi ili kulikamilisha hili. Suluhu ya mgogoro huu ni dhahiri iko mikononi mwa Myanmar na watu wa Myanmar.”

Mkuu wa IOM William Swing.
IOM/Amanda Nero
Mkuu wa IOM William Swing.

Kwa upande wake mkuu wa IOM William Swing ameongeza kuwa

“kwa kuzingatia ukubwa wa dharura yenyewe na huduma za kibinadamu zinazohitajika kuhakikisha maisha ya watu hao yanalindwa , kuendelea kutolewa kwa msaada ni lazima.”

Image
Wakimbizi WaRohingya kambini nchini Bangladesh. Picha: WFP

Naye mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa Bangladesh Bi mia Seppo ameishukuru jamii ya Bangladesh kwa ukarimu wao akisema “Bila shaka kuna shukran kubwa za kutolewa kwa ukarimu wa fedha za kukabiliana na mgogoro huu. Lakini jumuiya ya kimataifa isisahau kitu kimoja, mfadhili mkubwa katika janga hili ni Bangladesh.”

Ombi hilo litakaloshughulikia changamoto zilizoleta pamoja mashirika zaidi ya 100 ya Umoja wa Mataifa, ya kitaifa na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali (NGO’s) linajumuisha mipango ya dharura kwa ajili ya wakimbizi wengine 80,000 wa Rohingya wanaotarajiwa kuwasili Bangladesh katika miezi michache ijayo.