Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata wawaacha njia panda wakimbizi wa CAR nchini Chad: UNHCR

Picha: IOM/2014/Sandra Black
IOM ikisajili wakimbizi kutoka CAR wanaowasili Chad.

Ukata wawaacha njia panda wakimbizi wa CAR nchini Chad: UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linaendelea kutiwa hofu na mustakhbali wa maelfu ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR waliosaka hifadhi Kusini mwa Chad tangu mwaka jana.

Kwa mujibu wa UNHCR wimbi hilo la wakimbizi ambao ni kubwa tangu mwaka 2014, wengi wao wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, malazi na fursa ya huduma za afya na kutoa changamoto kubwa kwa mashirika ya kibinadamu katika kuwasaidia kutokana na ukata unaoyaghubika mashirika hayo. Babar Baloloch ni msemaji wa UNHCR Geneva Uswis

(SAUTI YA BABAR BALOCH)

“Ofisi ya UNHCR Chad inahitaji kiasi cha dola milioni 149 mwaka huu kukidhi mahitaji ya haraka , na hadi sasa imepokea asilimia 2 tu ya kiasi hicho.

Desemba mwaka 2017 mapigano baina ya makundi yenye silaha Kaskazini Magharibi mwaka CAR yalisababisha watu 65,000 kuwa wakimbizi wa ndani katika mji wa Paoua na wengine 5,000 kwenye mji wa Markounda.

Na kuendelea kuzorota kwa usala  nchini humo kuliwalazimu watu wengine 22,180 kufungasha virago na kukimbilia nchi jirani ya Chad. UNHCR inasema kwa ujumla watu 632, 000 wanaohudumiwa na shirika hilo wanahitaji msaada wa kimataifa.