Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 40 ya watu duniani hawana maji ya kutosha-Ripoti maalum

Mtoto anakunywa maji kutoka bomba la maji
Imal Hashemi/TAIMANI FILMS/Benki Kuu ya Dunia
Mtoto anakunywa maji kutoka bomba la maji

Asilimia 40 ya watu duniani hawana maji ya kutosha-Ripoti maalum

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ajenda mpya ya mpango tekelezi kuhusu maji  imetolewa leo na jopo la ngazi ya juu.

Jopo hilo ni la viongozi wa nchi 11 pamoja na mshauri maalum. Mwenyekiti wake ni rais wa Mauritania Bi Ameenah Gurib Fakim na mwenyekiti mwenza ni rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto.

Mbali ya mmoja wa wenyeviti kutoka Afrika , bara hilo pia lina wawakilishi wengine wawili ambao ni Afrika Kusini  na Senegal.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema kuwa sasa viongozi duniani wametambua  kuwa tunakabiliana na mgogoro wa maji na kwamba tunahitaji kukadiria  upya jinsi ya kutathmini na kusimamia maji. Akipokea ripoti hiyo Bw Guteress amoenyesha umuhimu wa maji kwa mwanadamu

(SAUTI YA  ANTONIO GUTERRES)

“Asilimia sitini ya mwili wetu ni maji. Watu bilioni mbili duniani hawapati maji safi ilhali watu wengine bilioni 4.5 hawana  huduma za kujisafi na majitaka . Hii ina maanisha tunakabiliana na changamoto kubwa”

Ajenda mpya inatoa mwito wa kuwepo na mwelekeo tofauti wa kimsingi wa jinsi dunia inavyotumia maji ili  malengo ya maendeleo endelevu SDGs yaweze kufikiwa hususan lengo  namba sita.

Bw Guterres amesema kuwa mapendekezo ya jopo yanaweza  kusaidia kulinda vyanzo vya maji  ili  ndoto itimie  ya kupata maji ya kunywa  salama pamoja  na kuwa na maji safi kwa wote.

Ripoti ya jopo imegundua kuwa mgogoro wa maji una pande nyingi na kusema leo hii watu asilimia 40 duniani hawana maji ya kutosha huku watu takriban milion700 maisha yao  yatavurugika kutokana na uhaba wa maji ifikapo mwaka wa 2030. Isitoshe ripoti imegundua kuwa watu zaidi ya bilioni mbili wanalazimishwa  kunywa maji machafu .

Mpango tekelezi uliopewa jina la: kila tone ni muhimu:ajenda ya hatua ya maji, unatoa mapendekezo mengi  kama sehemu ya  ripoti kutoka kwa jopo lililoitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na  rais wa benki Kuu ya dunia mwaka 2016.