Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yazindua app ya kukabiliana na viwavijeshi Afrika

Viwavijeshi kwenye mashamba kusini mwa Afrika. Picha: FAO

FAO yazindua app ya kukabiliana na viwavijeshi Afrika

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la chakula na kilimo duniani FAO , leo limezindua huduma ya kimtandao yaani app, itakayosaidia wakulima  barani Afrika kugundua mapema na   kupambana na tatizo la viwavijeshi katika mimea.

Huduma hiyo ya simu iitwayo FAMEWS, katika mfumo wa app, inatoa tahadhari, na pia elimu ya kutosha kuhusu tabia na mabadiliko ya viwavijeshi na pia kutoa mbinu kwa wakulima Afrika  jinsi ya kukabiliana na wadudu hao mapema iwezekanavyo .

Keith Cressman ambaye ni afisa kilimo FAO na moja ya wanzilishi wa huduma hiyo kwa ushirikiano na mashirika wadau wa Umoja wa Mataifa amesema, huduma hiyo ya kimtandao inawawezesha wakulima kupata data na maendeleo ya viwavijeshi barani Afrika na pia kutoa taarifa kwa vyombo husika ili tatizo liweze kushughulikiwa mapema.

Katika hatua za mwanzo, FAO ilizindua utekelezaji huduma hiyo ya kimdandao huko Madagascar na Zambia , na baadaye zitafuata katika nchi mbalimbali zilizoko kusini mwa jangwa la sahara ambazo zipo katika mtandao wa kilimo chini ya usimamizi wa shirika hilo.

FAO katika ripoti yake inasema viwavijeshi tayari vimeathiri ma milioni ya heka ya mazao barani Afrika na  kutishia usalama wa chakula kwa zaidi ya watu milioni 300, hasa wakulima wadogo ambao wanaojitahidi kuvuna agalau  chakula ili kukidhi  mahitaji ya  familia zao.