Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wa Syria hawana haki kama wengine?

Watoto Syria wakisimama katika hema katika makazi yao kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Bab Al Salame, Aleppo, Syria. Picha: UNICEF / Giovanni Diffidenti

Watoto wa Syria hawana haki kama wengine?

Haki za binadamu

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao mahsusi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu hususan watoto nchini Syria. 

Akihutubia kikao hicho mjini Geneva, Uswisi, mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Syria Panos Moumtzis amesema kutwa kucha watoto wa Syria hususan eneo la Ghouta Mashariki sasa wanakabiliwa na mmiminiko wa makombora.

Amesema baada ya miaka mitano ya kuishi kwenye eneo lililozingirwa, sasa wanaishi kwenye mahandaki yaliyojaa kupindukia bila kufahamu kesho yao itakuwa vipi.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Syria Panos Moumtzis akihutubia waandishi wa habari kuhusu Syria.
Picha: UM/Jean-Marc Ferré
Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Syria Panos Moumtzis akihutubia waandishi wa habari kuhusu Syria.

Bwana Moumtzis amesema maelfu wengine wakiwa wameuawa katika mzozo huo wa Syria, kwa wale waliokwepa makombora, kiwewe cha kisaikolojia kitadumu kwenye fikra za watoto hao wakati wote wa uhai wao.

Mratibu huyo wa masuala ya kibinadamu Syria baadaye alizungumza na waandishi wa habari akifafanua kuwa..

(Sauti ya Panos Moumtzis)

“Mara nyingi tunazungumzia takwimu, lakini baada ya kuzungumza na hizi familia na wanawake waliopoteza watoto wao, naweza kuwaambia kuwa nyuma ya kila takwimu hizi za kusikitisha kuna simulizi za kutisha na za machungu ambazo familia hizi hivi sasa zinapitia.”

Image
Picha: WHO_EPA/Stringer
Mtoto atibiwa baada ya mashambulio ya kemikali nchini Syria (Maktaba).

Amehoji iwapo watoto wa Syria hawana haki akisema ingalikuwa ni katika nchi nyingine duniani, shambulio moja kwenye hospitali lingalisababisha wito wa kuchukuliwa hatua na uwajibikaji; nchini Syria, zaidi ya mashambulio 100 ya aina hiyo yamefanyika kwa mwaka mmoja pekee na hakuna dalili za kumalizika.

(Sauti ya Panos Moumtzis)

“Na kama kuna ujumbe wowote kutoka kwenye Baraza hii leo ni kwamba sasa yatosha. Tumeona kuwa hatuna maneno zaidi ya kueleza hali mbaya ilivyo. Hakuna lolote la kuhalalisha mashambulizi dhidi ya watoto au watu wafariki dunia kwa kukosa huduma ya afya iliyo umbali wa maili moja tu kutoka eneo walipo.”