Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW62 yaanza leo New York

Mama mkulima kama huyu hunufaika na vyama vya ushirika.(Picha:Dasan Bobo / World Bank)

CSW62 yaanza leo New York

Wanawake

Zaidi ya washiriki 8000 wanahudhuria mkutano huu wa wiki mbili na kinachoangaziwa zaidi ni mustakhbali wa mwanamke na msichana wa kjijini.

Mkutano wa 62 wa Kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW unaanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Maudhui ya mkutano huo wa wiki mbili ni changamoto na fursa katika kufikia usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake na wasichana waishio vijijini.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wanawake, UNWomen, Phumzile Mlambo-Ngucka amesema maudhui hayo yanazingatia ukweli kwamba kampeni nyingi za kumkwamua mwanamke na msichana zinaangazia zaidi wale waishio mijini.

“Kwa msingi wa kutokumuacha nyuma mtu yeyote ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nje. Moja ya michango mikubwa zaidi ya kufanikisha ajenda 2030 ni kuondoa ukosefu wa usawa unaokabili wanawake na wasichana waishio vijijini, ” amesema Bi. Mlambo-Ngucka.

Mkurugenzi huyo mtendaji wa UNWomen amesema kundi hilo limekuwa likihaha kuchomoza lakini jitihada zao bado hazijazaa matunda na ndio maana wameamua kuangazia mwaka huu.

Amesema kundi hilo lina dhima muhimu duniani kuanzia uzalishaji wa chakula hadi usambazaji bila kusahau jukumu lao la usimamizi na uendeshaji wa kaya.

Wakati wa mkutano mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo vikwazo vinavyokabili wanawake wa vijijini na mwelekeo bora ili wajikwamue.

Zaidi ya washiirki 8000 watahudhuria wakiwakilisha mashirika zaidi ya 1200 ya kiraia. Halikadhalika viongozi wa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na vijana.