Vita dhidi ya magonjwa ya mifugo vinasonga mbele-FAO

Magonjwa ya mifugo sasa mkakati umepatikana. (Picha:tovuti FAO)

Vita dhidi ya magonjwa ya mifugo vinasonga mbele-FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Magonjwa yanayoshambulia mifugo ni hatari si kwa afya ya binadamu pekee lakini pia hugharimu mabilioni ya dola na pia kudumaza uchumi.

Dennis Carrol, kutoka shirika la misaada ya kimaendeleo la Marekani USAID, amesema hayo wakati akifafanua ushirika kati yao na shirika la Umoja wa mataifa la chakula na kilimo, FAO kabla ya mkutano wao huko Roma, Italia.

Amesema ni kwa kuzingatia gharama hizo za magonjwa ya mifugo kwa binadamu na uchumi ndio maana USAID na FAO wanalenga kukabiliana na magonjwa ya mifugo.

(Sauti ya Dennis Carrol)

“Tunajua kwamba ukiokoa maisha ya wanyama na kuhakikisha mifugo inaishi salama kiafya, hapo huwa sio tu tunazingatia usalama wa chakula lakini pia kuimarisha uchumi imara , na hivyo kuwa na jamii imara na yenye afya bora.”

Naye afisa kutoka FAO,Juan Lubroth, amenukuliwa akisema kuwa magonjwa mapya 75 ya kuambukiza ya binadamu ambayo yamejitokeza  katika miongo ya karibuni, chanzo chake ni mifugo.

Amesema ndio maana kuboresha mbinu za kugundua  na kukabiliana na magonjwa ya wanyama ni mkakati bora.

Mkutano wa Roma kati ya FAO na USAID unaleta pamoja wataalamu wao wakitathmini wamefika wapi katika juhudi zao za kukabiliana na magonjwa yanayoshambulia wanyama pamoja na wanadamu.