Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Liberia imarisha uhuru wa vyombo vya habari

Chapisho katika tovuti ya UNESCO ikioanisha uhuru wa vyombo vya habari na amani.(Picha:Tovuti ya UNESCO)

Liberia imarisha uhuru wa vyombo vya habari

Haki za binadamu

Uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na uwazi wa serikali ni miongoni mwa mambo ambayo Liberia inapaswa kuyapatia kipaumbele ili kuendelea kufaidi matunda yaliyopatikana baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu usongeshaji na ulinzi wa haki za kujieleza na kutoa maoni, David Kaye amesema hayo baada ya kuhitimiza ziara yake nchini humo.

Amesema azma ya serikali mpya chini ya Rais George Weah ya kusongeza haki hizo ni lazima ziungwe mkono, lakini serikali hiyo nayo lazima ichukue hatua kukamilisha hatua za awali za kulinda uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Mathalani amesema lazima Liberia ibadili sheria yake inayoharamisha kashfa kupitia vyombo vya habari pamoja na kubadili hadhi ya chombo cha utangazaji cha serikali kuwa shirika huru la umma la utangazaji.

Bwana Kaye amesema miswada ya sheria ya kubadili mambo hayo mawili  iko bungeni na hivyo ipitishwe haraka ili kuashiria azma ya Liberia ya kuzingatia sheria za kimataifa.

Amesema kwa kufanya hivyo, kauli ya Rais Weah kuwa Liberia iko tayari kimataifa itakuwa ni ya vitendo.

Wakati wa ziara hiyo ya wiki moja, Bwana Kaye alikuwa na mazungumzo na wadau mbalimbali wa serikali na kiraia akiwemo Rais Weah.