Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi ukizidi tokeni uwanjani- Zeid

Didier Yves Drogba Tébily, mwanasoka mashukuru duniani kutoka Côte d’Ivoire.
UN/maktaba
Didier Yves Drogba Tébily, mwanasoka mashukuru duniani kutoka Côte d’Ivoire.

Ubaguzi ukizidi tokeni uwanjani- Zeid

Haki za binadamu

Baadhi ya mashabiki wa mpira wamekuwa wakiwatupia wachezaji wa soka kauli za kibaguzi pindi wanapokuwa uwanjani. Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amesema hana uhakika ni hatua gani zimechukuliwa hadi sasa na shirikisho la soka duniani, FIFA kudhibiti vitendo hivyo dhalili, lakini wachezaji wenyewe wana uwezo mkubwa wa kutokomeza vitendo hivyo.

Wachezaji mpira wanapokumbwana kauli za kibaguzi kutoka kwa mashabiki uwanjani, wachukue hatua ikiwemo kutoka uwanjani, amesema Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi Bwana Zeid amenukuu mazungumzo yake na mwanasoka wa kulipwa nchini Ujerumani mwenye asili ya Afrika Kevin Prince Boateng, aliyemweleza kuwa ubaguzi viwanjani bado umeshamiri.

(Sauti ya Zeid Ra’ad Al Hussein)

“Wanacheza mchezo unaohusisha kupiga yaani kupiga mpira, sasa katika hali hiyo wao wenyewe wanaweza kujikuta wakipigwa au kushambuliwa na mashabiki na iwapo makamisaa wa mchezo hawafanyi lolote dhidi ya hilo basi  mtu anatumai kuwa wachezaji wenyewe wanaweza kujisimamia, wakaungana na kuchukua hatua na hata kutoka  uwanjani.”

Kamishna Zeid amesema wachezaji wengi wana wafuasi lukuki kwa hivyo kwa kuchukua hatua hiyo wanaweza kubadili mtazamo na fikra za kibaguzi dhidi ya wachezaji wa Afrika au wenye asili ya Afrika.