IOM itasimama kidete na wanawake wahamiaji popote walipo

Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya wanawake dunia, Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, limesema litasimama kidete kumtetea na kumlinda kila mwanamke au msichana mhamiaji mwenye moyo wenye wa matumaini, akili iliyojaa mawazo ya maendeleo popote alipo duniani.
Mkurugenzi wa IOM Wiliam Lacy Swing katika ujumbe wake siku ya wanawake yenye kaulimbiu “wakati ni sasa” amesema, bila kujali rika, kabila, rangi na hali ya kiuchumi, IOM pamoja na Umoja wa Mataifa wako bega kwa bega kuhakikisha kila mwanamke na msichana anaalindwa na kuwezeshwa katika dunia hii iliyojaa mfumo dume wanayokabiliana nao.
Halikadhalika bwana Swing amesema uwezeshwaji wa wanawake ni mwanzo kuinua jamii yote kwa ujumla, hivyo IOM inashirikiana na mamlaka zote za uhamiaji kuzuia na kupambana na aina zote za unyanyasaji na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana, na kushughulikia masuala mbalimbali ya kimuundo ambayo husababisha unyanyasaji huu na ubaguzi.
Ameongeza kuwa katika mazingira ya uhamiaji mwanamke ndie anaekabiliwa na majukumu makubwa ya kulinda na kuiwezesha jamii, katika kutafuta kazi, kulea watoto, na majukumu ya kifamilia mengine muhimu kuliko wanaume.
Katika maadhimisho ya leo IOM inasimama na wanawake wote katika heshima maalum kwa washirika wanaojitahidi kutetea haki za wanawake na wasichana. IOM itaendelea kusimama na wanawake wahamiaji kila uchao katika kuhakikisha haki inatendeka bila kujali hali zao.