Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubebeanaji mimba wageuza watoto bidhaa

Picha: UM/Maktaba
Mwanamke mjamzito.

Ubebeanaji mimba wageuza watoto bidhaa

Haki za binadamu

Ongezeko la kasi ya matukio ya wanawake kuingia makubaliano ya kubebeana mimba linatishia haki za mtoto, ameonya hii leo mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na unyanyasaji wa watoto, Maud de Boer-Buquicchio.

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi hii leo, Bi. Boer-Buquicchio amesema tishio hilo linazingatia ukweli kwamba kimataifa hakuna haki ya kuwa na mtoto na  hivyo mbebaji na mbebewaji wanaweza kuingia katika mvutano.

Amesema katika mazingira hayo watoto wanaozaliwa kupitia mfumo wa ubebeanaji mimba haki zao zinakumbwa na kizungumkuti hasa kwenye nchi ambako ubebeanaji mimba hufanyika kibiashara.

Mtaalamu huyo ameema iwapo mwanamke mbeba mimba analipwa ujira kwa kazi hiyo au mtu aliyeratibu mpango huo, hiyo ni biashara ya mtoto kwa mujibu wa sheria za haki za binadamu za kimataifa.

Kwa mantiki hiyo ametaka kuwekwa kwa mifumo ya kusimamia biashara hiyo ya ubebeanaji mimba kwa kuwa wahusika wataendelea kuhama kutoka eneo moja hadi jingi ili kukidhi matakwa yao huku haki za mtoto zikiendelea kusiginwa, akisema “Serikali bila kujali mtazamo wao kuhusu kitendo cha watu kubebeana mimba ni lazima ziweze mifumo ya kuzuia biashara au usafirishaji wa watoto kwa minajili hiyo.”