Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria ifikishwe mbele ya mahakama ya ICC: Zeid

Mtoto akiwa amebeba mfuko wenye kuni huko Ghouta Mashariki nchini Syria.
UNICEF/Al Shami
Mtoto akiwa amebeba mfuko wenye kuni huko Ghouta Mashariki nchini Syria.

Syria ifikishwe mbele ya mahakama ya ICC: Zeid

Amani na Usalama

Kamisha mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo ametoa wito wa mgogoro wa Syria kufikishwa kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.

Zeid Ra’ad al-Hussein ametoa wito huo mjini Geneva Uswis wakati wa mjadala wa dharura wa baraza la haki za binadamu kuzungumzia mgogoro wa Ghouta Mashariki ambako wakazi 400,000 bado wanazingirwa.

Zeid ameielezea hali ya eneo hilo kama “moja ya madhila makubwa ya kusikitisha” katika historia ya vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoshuhudia raia wakitolewa kafara au kuuawa.

Amegusia kwamba uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unafanyika Ghouta Mashariki na kwingineko Syria, akiongeza kuwa wahusika wote watawajibishwa.

Flora Nducha
Syria lazima ifikishwe mbele ya mahakama ya ICC: Zeid

(SAUTI YA ZEID)

“Syria ni lazima ipelekwe kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu. Majaribio ya kukwepa sheria na kuwafisha wahalifu ni aibu .Pia naziomba nchi zote kuongeza msaada wao kwa ajili ya chombo huru cha kimataifa, kisicho na upendeleo kilichoanzishwa mwaka jana. Wajibu wa chombo hicho  IIIM ni kuhakikisha kwamba taarifa kuhusu uhalifu zinakusanywa, kufanyiwa tathimini na kuhifadhiwa, kwa mtazamo wa maandalizi ya kufungua kesi baadaye. Kazi hii ni muhimu, na pongezi kwa kazi nzuri iliyofanywa na tume huru ya kimataifa ya baraza la haki za binadamu ya uchunguzi wa Siria. "

Image
Watoto Syria wajificha mlangoni huku kukiwa na milio ya risasi na makombora. Picha: UNICEF/NYHQ2012-0218/Alessio Romenzi

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema madhila wanayopitia watoto nchini Syria hayasemeki, ni kama wako jehanamu wakikosa huduma zote muhimu na za msingi.

Lakini sasa baada ya kutangazwa usitishaji mapigano kwa siku 30 UNICEF inasema ipo tayari na msaada wa kuokoa maisha zikiwemo dawa, lishe, kwa ajili ya watoto wenye utapia mlo , vifaa vya wakati wa kujifungua, nguo za baridi, vifaa vya usafi na bidhaa zingine za matumizi ya kawaida.