Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Japo wanakula nyama simba na jamii yake wastahili kulindwa: UN

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed. Picha: UM/Kim Haughton

Japo wanakula nyama simba na jamii yake wastahili kulindwa: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuna haja ya kuunda ushirika mpya  kati  ya serikali, makundi ya kulinda wanyama na mazingira pamoja na jamii katika juhudi za kushughulikia  ulinzi wa mazingira kama chanzo cha kujenga uchumi endelevu.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi.Amina J. Muhammed katika hafla iliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya Wanyama pori ambayo kila mwaka huwa Machi 3.

Image
Chui nchini India.(Picha:UM/John Isaac)

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inahusu wanyama wakubwa aina ya paka kama Simba, Chui, Simba marara ama wengine wanamuita Chui mkubwa, Duma, Puma na wanyama wengine ambao  wanakabiliwa na vitisho vya kutoweka. Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu asema yanawalenga Wanyama wakubwa wanaowinda maarufu kama Paka wakubwa.

(SAUTI YA AMINA .J. MOHAMMED)

“ Tangu zamani, wanayama hawa paka wakubwa, wametoa nembo maarufu duniani za nguvu, uzuru, na madaha.  Tunaona hiyo tunu katika  nembo ambazo huchaguliwa na makampuni yanayotengeneza magari au vyombo vya michezo. Pia tunaona katika mitindo, vitabu vya watoto, na pia katika sinema. Licha ya hayo viumbe hawa wako katika hatari ya kutoweka. Paka wakubwa wamekuwa wakipungua kwa kasii. Karne moja tu iliyopita katika bara la Asia kulikuwa na Simba marara 100,000.”

Simba anaangalia mazingira yake nchini Kenya.
Photo: UN/DPI Photo
Simba anaangalia mazingira yake nchini Kenya.

Ameongeza kuwa leo wamebaki takriban 4,000 na wamepoteza asilimia 96 ya makazi yao asilia, na kusema kuwa sisi binadamu tumechangia hiyo  na hivyo tunaweza pia kuwa waokozi wa hali hiyo. Amekumbusha kuwa moja wa malengo ya maendeleo endelevu kuna vipengee vinavyolenga  kukomesha  uwindaji haramu, usafirishaji wa magendo wa wanyama pori ambao wanalindwa.