Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na tembo kulindwa Bangladesh: UNHCR

Wakimbizi WaRohingya kambini nchini Bangladesh. Picha: WFP

Wakimbizi na tembo kulindwa Bangladesh: UNHCR

Amani na Usalama

Kikosi kazi maalumu kimeundwa nchini Bangladeshi ili kuhakikisha usalama wa maelfu ya wakimbizi wa Myanmar na tendo ambao sasa wanaranda kwenye makazi ya wakimbizi hao. 

Kikosi kazi hicho kimeundwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Muungano wa kimataifa wa hifadhi ya mali asili ili kuzuia matukio ya hatari baina ya tembo na binadamu katika moja ya makazi makubwa kabisa ya wakimbizi duniani baada ya tukio la karibuni la watu kukanyagwa na tembo kambini hapo kusababisha vifo 10.

Tembo hao wa Asia walio hatarini kutoweka wakiwa katika safari zao za kawaida kati ya Bagladesh na Myanmar wamekuwa wakiranda kwenye makazi ya wakimbizi na kuharibu vitu, kuua na kujeruhi watu.

Kikosi kazi hicho kitashirikiana na wote , wakimbizi na jamii zinazowahifadhi kwa kushirikisha idara ya misitu ya Bangladesh na ofisi ya kamishina ya misaada na usafirishaji wa wakimbizi.

Baadhi ya hatua zinazochukuliwa na kikosi kazi hicho ni kuweka minara ya uangalizi kuzunguka makazi ya wakimbizi , kuweka timu maalumu itakayotoa tahadhari wakati tembo akiinga kwenye makazi na pia kuweka alama kwenye njia zote tembo wanakopita ili watu waziepuke.