Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel msiwaondoshe kwa shuruti Waeritrea na wasudan:UN

Wakimbizi wa Eritrea, Sudan na Egypt wakimbia nchi zao kuelekea nchi jirani ikiwemo Syria. Picha: UNHCR

Israel msiwaondoshe kwa shuruti Waeritrea na wasudan:UN

Amani na Usalama

Sera mpya ya Israel ya kuwaondoa nchini humo kwa nguvu raia wa Eritrea na Sudan inakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na wakimbizi wamesema wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu.

Wataalamu hao ambao wametoa wito kwa Israel kusitisha mara moja, kubadili sheria hiyo na utekelezaji wake, wamesema chini ya sheria hiyo, maelfu ya raia wa Eritrea na Sudan ambao ndio sehemu kubwa ya raia wa kigeni wanaoomba hifadhi Israel watapelekwa kwa shuruti katika mataifa ya tatu yasiyojulikana.

Serikali ya Israel imearifiwa kuanza kutoa angalizo la watu kuondolewa tangu tarehe 4 Februari mwaka huu na taarifa za karibuni zikisema takribani raia saba wa Eritrea wanashikiliwa kwa muda usiojulikana kwa kugoma kuondolewa kwa nguvu nchini humo.

Wataalamu hao wanasema hofu yao ni kwamba será hiyo na utekelezaji wake unakiuka kwa kiasi kikubwa haki za Waeritrea na Wasudan hao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, wakimbizi, kazi na ubinadamu.

Ingawa sera hiyo inajumuisha kusamehewa kwa muda kwa baadhi ya watu wakiwemo wahamiaji wa makundi yasiyojiweza, lakini wataalamu wanahofia hatua hiyo inaweza kuondolewa na fukuza hiyo ikawakumba pia watoto, familia na watu ambao maombi yao ya hifadhi bado hayajashughulikiwa.

Hivi sasa Wasudan na Waeritrea 20,000 kati ya 34,700 wanashinikizwa kuchagua ama kuondolewa nchini humo au kuswekwa rumande Israel kwa muda usiojulikana.