Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madini ya joto (Iodini) ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto-UNICEF

Mtoto mchanga. Picha: UNICEF

Madini ya joto (Iodini) ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto-UNICEF

Afya

Chumvi yenye madini ya joto au iodini kwa ukuwaji wa mtoto ni muhimu sana kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF likishirikiana na shirika la GAIN.

Ripoti hiyo inasema takriban watoto milioni 19 ambao ni swa na asilimia 14 ya watoto wanaozaliwa kila mwaka, wako hatarini kupata matatizo ya ubongo kutokana na uhaba wa madini joto au Iodini mwilini mwao, madini ambayo yanapatikana kwenye chumvi.

Mshauri mkuu wa UNICEF wa masuala ya lishe, Ronald Kupka, anasema lishe apatayo mtoto katika kipindi chake cha mwanzo wa maisha yake inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa ubongo wake hali ambayo inaweza kumuendeleza au kutia dosari maisha yake ya hapo baadae.

Mbali na hayo, wataalam wanasema madini joto ni muhimu kwa mwanadamu kwani mwili wake unahitaji iodini na aslimia kubwa ipo katika chakula cha kawaida au maji. Uhaba wa iodini unasababisha  maradhi kadhaa ikiwemo tezi la shingo.

Ripoti hiyo, yenye kichwa: “Mustakhbali bora , kulinda maendeleo ya awali ya ubongo kupitia chumvi ya madini ya joto” inabaini kuwa  uhaba wa madini joto ndio sababu kuu, inayozuilika, ambayo huathiri maendeleo ya ubongo wakati wa miaka ya mwanzo ya maisha ya mwanadamu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa será ya chakula katika shirika la GAIN, Greg S. Garret, akisisitiza umuhimu wa madini hayo Kusini mwa bara Asia ni la pili duniani kwa kiwango kikubwa cha chumvi yenye madini joto, huku maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kukukiongoza kwa uhaba wa madini hayo na ambapo asilimia 25 ya watu hawapati chumvi yenye iodini na kuwaweka watoto milioni 4 hatarini kila mwaka.