Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechode wasichana waliotekwa Nigeria warejeshwe- UN

Picha ya maktaba ya UM
Moja ya matembezi ya kushinikiza kuachiliwa kwa wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram (maktaba).

Chondechode wasichana waliotekwa Nigeria warejeshwe- UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa juu ya hatma ya zaidi ya wasichana 100 nchini Nigeria ambao yadaiwa walitekwa nyara na Boko Haram wiki iliyopita.

Wasichana hao ni  wa shule ya sekondari ya Bursari inayomilikiwa na serikali iliyoko mji wa Dapchi jimbo la Yobe, kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka watoto hao waachiliwe huru mara moja bila masharti yoyote huku akilaani vikali kitendo hicho cha kushambulia shule yao na kuwateka nyara.

Ametoa wito kwa mamlaka nchini Nigeria kuhakikisha watoto hao wanarejeshwa na kuunganishwa na familia zao na kutaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Ameelezea mshikamano wa Umoja wa Mataifa na serikali na watu wa Nigeria na ukanda mzima wa Afrika Magharibi katika kukabiliana na ugaidi na misimamo mkali.

Wakati huohuo, Virginia Gamba ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto walio kwenye mizozo, amelaani vikali kitendo cha wasichana hao kutekwa nyara akienda mbali zaidi kuangazia uharibifu wa miundombinu ya elimu.

“Mashambulizi dhidi ya shule yameendelea kuripotiwa kaskazini-mashariki mwa Nigeria”, amesema Bi. Gamba akiongeza kuwa yakadiriwa shule 1,400 zimeharibiwa tangu kuanza kwa mashmbulizi ya Boko Haram mwaka 2009.

“Kwa kiasi kikubwa mashambulizi yamejikita katika utekaji nyara, utumikishaji wa lazima kwenye mapigano, mauaji na kukata viungo pamoja na ukatili wa kingono kwa wasichana wa Nigeria ambao kosa lao tu ni kuzaliwa wanawake na ndoto ya kupata elimu”, anahitimisha Bi Gamba katika taarifa yake akisema kuwa sasa vitendo hivyo lazima vikome.