Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi watumikishwa jeshini Yemen

Rahaf Ali Bedaish, msichana mwenye umri wa miaka 8 anabeba ndugu yake Ahmed, mwenye umri wa miaka 2 kambini Dharawan.  Wamepoteza makazi yao huko Taizz tangu mizozo ianze Yemen.
UNHCR/Mohammed Hamoud
Rahaf Ali Bedaish, msichana mwenye umri wa miaka 8 anabeba ndugu yake Ahmed, mwenye umri wa miaka 2 kambini Dharawan. Wamepoteza makazi yao huko Taizz tangu mizozo ianze Yemen.

Watoto zaidi watumikishwa jeshini Yemen

Amani na Usalama

Kadri siku zinavyosonga hali ya kibinadamu nchini humo inazidi kuwa tete huku mapigano yakiendelea raia wakigharimika zaidi. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejulishwa hii leo huku  likipatiwa mambo matatu ya kipaumbele ili kushughulikia janga hilo linaloelezwa kuwa ni kubwa zaidi la kibinadamu duniani.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed ameelezea masikitiko yake juu ya ripoti ya kwamba pande kinzani nchini humo zinatumikisha maelfu ya watoto kwenye vikundi vyao vya mapigano.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo ikiwa ni mara ya mwisho kabla ya kuhitimisha jukumu lake, Bwana Ahmed amesema utumikishaji wa watoto umeripotiwa na mashirika ya misaada ya kibinadamu na unatekelezwa na serikali ya Yemen na kundi la wahouthi.

(Sauti ya Ismail Ould Cheikh Ahmed)

“Wakati ripoti zinadokeza kuwa pande zote kinzani zinatumikisha watoto, mfumo maalum wa wahouthi kutumikisha watoto jeshini unaweza kuwa madhara kwa mustakhbali wa nchi hiyo.”

Akihutubia Baraza hilo kuhusu hali ya kibinadamu nchini Yemen, Mkurugenzi wa Operesheni za ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu OCHA, John Ging amesema janga la kibinadamu Yemeni ni kubwa zaidi kuliko majanga yote duniani  hivi sasa.

(Sauti ya John Ging)

“Maisha ya watu yanaendelea kudorora. Mzozo unazidi kushika kasi tangu mwezi Novemba na kusababisha awtu wapatao 100,000 wakimbie makazi  yao, hiyo ni kwa mujibu wa UNHCR. Watu wengi zaidi wanashindwa kupata mlo, njaa kali inasalia kuwa tishio kubwa. Ijapokuwa visa vya kipindupindu vinapungua, ugonjwa huo bado haujadhibitiwa na unaweza kurejea tena msimu ujao wa mvua.”

Bwana Ging ametaja mambo matatu muhimu yanayohitajika sasa kuimarisha usaidizi ambayo ni mosi, kupata fedha kujazia ombi la dola bilioni 2.9 kwa ajili  ya usaidizi wa Yemen.

Pili ni hakikisho la usalama ili kufikisha mahitaji ya kibinadamu kwa wananchi hasa maeneo yaliyozingirwa na tatu ni kuondolewa kwa vikwazo vinavyochelewesha vibali kwa meli za kibiashara zenye shehena za vyakula na petroli kutia nanga bandari za Hudaydah na Saleef nchini Yemen.