Mlipuko wa kipindupindu wadhibitiwa miongoni mwa wakimbizi, Uganda

Licha ya idadi ya wakimbizi walioambukizwa maradhi ya kipindupindu nchini Uganda kuongezeka hadi 949 kutoka takribani wagonjwa 700 Ijumaa iliyopita, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, nchini humo limesema mlipuko huo umeanza kudhibitiwa.
Afisa mwandamizi wa uhusiano wa UNHCR nchini Uganda Joyce Munyao-Mbithi amesema kiwango cha maambukizi sasa hakitishi kama ilivyokuwa katika siku za kwanza za mlipuko huo ambao umeingia wiki ya pili.
Amesema, kuna kifo kimoja tu kilichosajiliwa tangu Ijumaa wiki jana, kinachofikisha jumla ya vifo 27 tangu mlipuko huo uanze.
Bi. Mbithi amesema hali hiyo ni matunda ya juhudi za wadau mbalimbali wa Umoja wa Mataifa ikiwemo serikali ya Uganda kudhibiti mlipuko huu, juhudi ambazo ni pamoja na uhamasishaji, na uwepo wa huduma thabiti za usafirishaji na usimamizi wa wathirika kambini na katika jamii za wananchi.
Mmoja wa wakimbizi anasubiri kwa hamu mwanae apone ili aelekee kituo cha wakimbizi cha Kyangwali.
(Sauti ya Mkimbizi)
Habari hizi chanya zinapokewa wakati idadi ya wanaokimbia vurugu za kikabila Jimboni Ituri nchini Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, imepungua hadi watu wasiozidi 100 kwa siku ikilinganishwa na zaidi ya 300 siku chache kabla na baada ya mlipuko wa kipindupindu.