Shughuli za kisiasa Burundi zimebinywa- Kafando

26 Februari 2018

Nchini Burundi,  sintofahamu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyoanza baada ya Rais Pierre Nkurunzinza kuongeza muda wa uongozi na kuingia awamu ya tatu bado inaendelea na sasa yaelezwa kuwa shughuli za vyama vya kisiasa zinaendeshwa na watu wachache.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi, Michel Kafando amesema hali ya kisiasa nchini humo bado ni tete.

Akihutubia Baraza la Usalama wakati wa kikao mahsusi kuhusu nchi hiyo ya Maziwa Makuu, Bwana Kafando amesema hali ya kisiasa ni tete kwa sababu ni chama kikubwa pekee cha kisiasa nchini humo pamoja na washirika wake ndio wanaoweza kufanya shughuli za kisiasa.

Kuhusu uchumi amesema hali tete ya kisiasa inakwamisha kukwamuka kwa uchumi wa Burundi ingawa akisema kuna nuru kwenye hali ya usalama.

Hata hivyo hali ya haki za binadamu bado kuna shida, hivyo amesema.

(Sauti ya Michel Kafando)

“Kuna lengo moja linaloongoza vitendo. Kupaza sauti ili mustakhbali unaojengwa na warundi uwe ni ule ambao unaungwa mkono na warundi wote, na hivyo kuepuka mkwamo na shida ambazo warundi wamekumbana nazo kupita kiasi.”

Kuhusu uchaguzi wa mwaka 2020, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu ujenzi wa amani Burundi, Balozi Jürg Lauber amesema.

(Sauti ya Balozi Jürg Lauber)

“Chaguzi zijazo mwaka 2020 zinahitaji uangalizi mkubwa wa kimataifa. Itakuwa mafanikio makubwa iwapo wadau wa kitaifa, kikanda na kimataifa watakubaliana juu ya mpango ili kuweka mazingira yanayohitajika ya kuwa na chaguzi za kidemokrasia, amani na jumuishi mwaka 2020.”

Mzozo nchini Burundi ulianza mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunzinza kusaka awamu ya tatu ya uongozi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter