Wakimbizi wauawa na wengine kujeruhiwa Rwanda, UNHCR yashtushwa

23 Februari 2018

Wakimbizi watano kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC wameuawa na wengine  wengi, mkiwemo afisa wa polisi kujeruhiwa, wakati vikosi vya usalama vilipokuwa vinajaribu kuzima maandamano ya wakimbizi wa kambi ya  Kiziba  magharibi mwa Rwanda. 

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR lasema limeshtushwa na taarifa za vifo vya wakimbizi hao nchini Rwanda.

Msemaji wa UNHCR, Cecile Pouilly, amewataka wahusika nchini Rwanda kuhakikisha usalama wa wakimbizi baada ya  maandamano yaliyokuwa yakiendelea tangu Febuari 20 kusababisha vifo na majeruhi na kuongeza kuwa

(SAUTI YA CECILE POUILLY)

“ Tunasikitika kwamba licha ya kuendelea kuomba watu kujizuia na kudumisha utulivu ombi halikuheshimiwa. Mkasa huu ungeepukwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wakimbizi hayakubaliki, UNHCR inatoa wito kwa mamlaka kujizuia na matumizi Zaidi ya nguvu na kuchunguza mazingira ya tukio hilo.”

Taarifa zasema kuwa mkasa huo ulitokea baada ya takriban wakimbizi 700 wa DRC kutoka kambi ya Kiziba  kuandamana nje ya ofisi ya UNHCR sehemu za Karongi kupinga kupunguzwa mgao wao wa chakula. Katika hali ya kuzima maandamano hayo, polisi inaripotiwa kutumia vitoa machozi baada ya juhudi kuzuia maandamano kushindwa. Baadae inaripotiwa kutzuka  purukushani na polisi kuwafyatulia risasi  za moto waandamanaji waliokuwa wamejawa na hasira.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter