Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili gani wasubiriwa ili hatua zichukuliwe huko Ghouta?

Familia ikihamisha vifaa vyake kwa kutumia tololi wakati ikikimbia kutoka eneo lenye mapigano huko Ghouta Mashariki nchini Syria.
UNICEF/Amer Al Shami
Familia ikihamisha vifaa vyake kwa kutumia tololi wakati ikikimbia kutoka eneo lenye mapigano huko Ghouta Mashariki nchini Syria.

Ukatili gani wasubiriwa ili hatua zichukuliwe huko Ghouta?

Amani na Usalama

Syria hali inazidi kuwa mbaya zaidi , raia wanakabiliwa na mashambulizi. Tangu tarehe 4 mwezi huu wa Februari raia zaidi ya 300 wameuawa kwenye mapigano kati ya serikali na wapinzani.

Umoja wa Mataifa umeendelea kupazia sauti ili kukomeshwa kwa ukatili dhidi ya raia kwenye eneo la Ghouta mashariki nchini Syria.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye mjadala wa wazi wa Baraza Kuu alielezea masikitiko  yake juu ya mazingira ya kutisha na ya kikatili wanamoishi raia akisema ni sawa na jehanam duniani.

Ametaka pande zote kinzani kwenye mzozo wa Syria kusitisha mapigano akisema anaunga mkono mashauriano yanayoendelea ili kukomesha mapigano lakini ifahamike kuwa wakazi wa Ghouta mashariki hawawezi kusubiri.

Wakati huo  huo Kamisha Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Raad al Hussein amehoji ni kiasi gani cha ukatili kinasubiriwa kuwakumba wananchi wa Syria kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua.

Amesema tangu serikali ya Syria ianze mashambulizi yake makali dhidi ya eneo la Ghouta mashariki linalokaliwa na upinzani tarehe 4 mwezi huu, watu 346 wameuwa na 92 kati  yao ni siku ya Jumatatu pekee.

Amerejelea wito Umoja wa Mataifa wa kutaka mapigano yakome ili huduma za kibinadamu ziwafikie raia.

Bwana Zeid amesema makubaliano yoyote ya sitisho la mapigano lazima yazingatie sheria za kimataifa za kibinadamu ikiwemo kuhakikisha hakuna watu wanaolazimishwa kuhama.