Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi nchini Rwanda wagoma, UNHCR yasema tulieni

(Picha:UNICEF/NYHQ2015-1378/Pflanz)
Watoto wakimbizi katika kambi moja nchini Rwanda.

Wakimbizi nchini Rwanda wagoma, UNHCR yasema tulieni

Amani na Usalama

Nchini Rwanda, wakimbizi katika kambi ya Kiziba magharibi mwa nchi hiyo wameandamana kupinga kupunguzwa kwa mgao wa chakula.

Kumetokea vurugu katika kambi moja ya wakimbizi  kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, waishio nchini Rwanda zikihusiana na mgao wa chakula. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema wakimbizi katika kambi ya Kiziba, iliyoko  wilaya ya Karongi, magharibi mwa Rwanda, waliandamana wakidai mgao wa kutosha wa chakula baada ya mgao kupunguzwa. Walinzi kambini hapo walifyatua risasi ili kuwatawanya.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Rwanda, Ahmed Baba Fall amesema kuwa kipaumbele kwao ni ulinzi na usalama wa wakimbizi, na kuwaomba wakimbizi kufuata sheria za nchi ambapo inaarifiwa kuwa baadhi ya wakimbizi, kwa kukatishwa tamaa, walionyesha nia ya kurejea  DRC.

Kambi hiyo ina wakimbizi 17,000 kutoka DRC na asilimia 77 ni watoto na wanawake.

Shughuli za msaada wa kibinadamu nchini Rwanda zinakabiliwa na ukata kiasi cha kulazimika shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, kupunguza  mgao wa chakula mara mbili.

Mwezi novemba mwaka 2017 mgao ulipunguzwa kwa asilimia 10 ilhali januari mwaka 2018 asilimia nyingine 25.

Ombi la UNHCR kwa mwaka 2018 la dola milioni 98.8 kwa minajili ya kuwasaidia wakimbizi walioko Rwanda hadi sasa limefadhiliwa kwa asilimia 2 tu.