Katiba ya UN iende na wakati ili kukidhi mahitaji- Guterres

21 Februari 2018

Kupatia suluhu changamoto kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji na ukosefu wa usawa ni majaribio makubwa sana kwa Katiba ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha dunia inakuwa bora kwa watu wote.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa hii leo jijini New York, Marekani wakati akihutubia Mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ku husu malengo na misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa katika kuendeleza amani na usalama duniani.

Amesema ni dhahiri kuwa Katiba hiyo au chata iliyoanzisha Umoja wa Mataifa mwaka 1945 imepitia majaribu mengi na kupatia suluhu mambo mengi lakini..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Ingawa misingi ya katiba inakwenda na wakati kuliko wakati wowote ule, ni lazima tuendelee kuboresha mbinu zilizomo, na ni lazima tuzitumie kwa azma kubwa, na lazima turejelee misingi  ya kutungwa katiba hiyo tunapohaha kuhudumia wakazi wa dunia.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres akihutubia Baraza la Usalama.
UN /Loey Felipe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Baraza la Usalama.

Bwana Guterres ametolea mfano suala la ulinzi wa amani akisema halipo kwenye Katiba lakini linatekelezwa kwa kutumia vipengele vilivyomo.

Mjadala huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye amesema kuwa dunia imebadilika na hata baadhi ya watu wanahoji dhima ya Umoja wa Mataifa katika kulinda amani na usalama duniani.

Amesema hoja hizo zinajibika kwa jinsi chombo hicho kilivyosaidia kutatua mizozo iliyoibuka duniani katika kipindi cha uwepo wake kwa zaidi ya miaka 70.

Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala kuhusu uendelezaji wa amani na usalama duniani Februari 2018
UN /Loey Felipe
Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala kuhusu uendelezaji wa amani na usalama duniani Februari 2018

Hata hivyo Bwana Ban amesema ili Umoja wa Mataifa uweze kushughulikia ipasavyo changamoto za kiusalama zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, ugaidi, misimamo mikali na uendelezaji wa nyuklia..

(Sauti ya Ban Ki-moon)

“Baraza la Usalama ni lazima lifanyiwe marekebisho ili liweze kwenda na wakati katika mchakato wake wa kupitisha uamuzi. Marekebisho ya Baraza la Usalama yamechelewa mno. Tunapaswa kujikumbusha kuwa wajibu wa msingi wa kulinda amani na usalama uko ndani ya nchi wanachama wenyewe.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter