Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana lazima wawezeshwe ili kufanikisha SDGs: UN

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Bi Amina J. Mohammed akihutubia mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya SDGs mjini Minsk Belarus.
Umoja wa Mataifa/Egor Dubrovsky
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed akihutubia mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya SDGs mjini Minsk Belarus.

Vijana lazima wawezeshwe ili kufanikisha SDGs: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mataifa yanayoendelea yameshauriwa, miongoni mwa mambo mengine, kuwawezesha vijana na  pia kuhakikisha usawa wa  kijinsia ili kufanikisha  malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Bi Amina J. Mohammed akihutubia mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya SDGs mjini Minsk Belarus.

Bi Mohammed amewataka wajumbe wa mkutano huo kusonga mbele na ufanikishaji wa malengo hayo huku akisisitiza kwamba kila jamii ni lazima ijumuishwe.

Akiwahutubia wajumbe mbalimbali wanaokutana kutafuta njia za kufanikisha malengo hayo, amesema masuala ya haki na kuwashirikisha vijana na wanawake katika upangaji pamoja na utekelezaji wa sera ni muhimu mno akiongeza kuwa wakati umefika kuacha mienendo  isiyofaa kama vile kunyanyapaa,  na ubaguzi,  akikariri, kuwa ni sharti wahakikishe kila mmoja anapata haki zake inavyostahili.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Bi Amina J. Mohammed akihutubia mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya SDGs mjini Minsk Belarus.
Umoja wa Mataifa/Egor Dubrovsky
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed akihutubia mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya SDGs mjini Minsk Belarus.

Bi Mohammed amesema kuwawezesha vijana na pia suala la usawa wa kijinsia ni moja wa vipengele ambavyo vinasaidia kuleta maendeleo kwani kazi ya kufanikisha malengo hayo endelevu inahitaji serikali kuweka mikakati yao upya na pia kutafuta ufadhili, teknolojia zinazohitajika pamoja na wataalamu.

Mapendekezo ya mkutano huo yatawasilishwa katika  mkutano wa kikanda wa maendeleo endelevu wa tume ya maendeleo ya  kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa bara la Ulaya utakao fanyika mjini Geneva wiki ijayo.