Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kuporwa hospitali ya Tonga, huduma ni mtihani: UNMISS

Walinda amani wa UNMISS wakiwasaidia raia wanokimbia machafuko jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.(Picha:UNMISS)

Baada ya kuporwa hospitali ya Tonga, huduma ni mtihani: UNMISS

Ujumbe wa Umoja wa mataifa Sudan Kusini-UNMISS-yasema kuwa  mji wa Tonga ulioko katika eneo la Upper Nile unahitaji msaada wa huduma za kiafya baada ya makundi yanayohasimiana kupora kituo pekee cha cha kiafya katika eneo hilo.

Mji wa Tonga unapatikana katika eneo la Upper Nile Sudan Kusini. Jamii za eneo hilo zilitoroka mapigano yalipoanza kati ya jeshi la Sudan Peoples Army-SPLA- dhidi ya vikosi vya upinzani.

Nyumba zilichomwa, shule zikafungwa na vituo vya afya kuhujumiwa na hivyo kusababisha raia kadhaa kupoteza maisha yao.

Kituo cha afya cha Tonga  ndicho kituo pekee kinachotoa huduma za kiafya katika eneo hilo, lalini kituo cha afya kimebaki jina tu kwani ni kitupu sasa hamna lolote. Makundi yanayohasimiana yalipora vifaa vyake karibu vyote kama vile vitanda, vifaa vingine  na pia madawa.

Ujumbe wa  Umoja wa Mataifa Sudan Kusini-UNMISS- unasema kituo hicho cha afya kinafanya kazi sasa lakini uwezo wake ni wa chini sana.Kila siku hupata wagonjwa kati ya watano na 13 na wagonjwa wengi ni kutokana na homa ya malaria, kuharisha, homa ya matumbo, na magonjwa mengine yatokanaayo na maji machafu.


Kikosi cha ujumbe wa UNAMISS hivi majuzi kilitembelea eneo hili ambalo linadhibitiwa na wapinzani wa serikali ili kuona hali ya kiusalama ilivyo na pia kuona mahitaji ya msaada wa kibnadamu.David Shearer , ni mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.

(Sauti ya Dkr Shearer)

“Kutokana na yale tuliyojionea ni kweli kuna haja.Watu wanahitaji huduma. Sasa kile tunachofanya ni kuona jinsi gani tunaweza kushughulikia haja hiyo kutoka kwa kazi zetu tunazofanya  katika maeneio mengine ya nchi”.

Ujumbe wa UNMISS unasema kituo hicho cha afya, baado ni tegemeo kubwa lililobaki kwa wananchi wa eneo la Tonga  kuweza kupata msaada.

Aliza Nyaluit Lowal, mama mwenye umri wa miaka 27,  hana mme na ana watoto wanne, peke yake, akiwa amebeba mtoto wake mgonjwa wa miezi 14  alitembea mwendo wa saa 11(kumi na moja) kupitia maeneo hatari hadi kituoni hapo lakini kilikuwa kitupu.

(Sauti ta Alisa Lowai)


“Tumekuwa tunakimbia miaka yote hii. Tunahitaji amani. Amani itarejelea lini Sudan Kusini?”