Janga kubwa la kibinadamu lanyemelea Tanganyika

Mnamo Januari 2017, takriban wakimbizi 50,000 waliokimbia mizozo Tanganyika waliwasili Kalemie ambako kwa sasa wanaishi katika hali ngumu zaidi.
OCHA
Mnamo Januari 2017, takriban wakimbizi 50,000 waliokimbia mizozo Tanganyika waliwasili Kalemie ambako kwa sasa wanaishi katika hali ngumu zaidi.

Janga kubwa la kibinadamu lanyemelea Tanganyika

Haki za binadamu

Janga kubwa la kibinadamu linanyemelea maeneo ya kusini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati huu ambapo eneo hilo linakumbwa na mapigano na ukiukwaji mkubwa wa kibinadamu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hayo hii leo likisema ukatili wa hali ya juu na ukimbizi wa ndani unaendelea kwenye jimbo la Tanganyika lililoko eneo hilo kutokana na mapigano ya kikabila baina ya makabila ya Twa, Luba na mengineyo.

Kama hiyo haitoshi raia wanakabiliwa na athari za mapigano kati ya jeshi la serikali ya DRC na vikundi vilivyojihami tangu mwezi Januari huku makundi mengine nayo yakitishia kuibua zahma.

Simulizi za watu waliosaka hifadhi kwenye mji mkuu wa jimbo la Tanganyika, Kalemie ni pamoja na kubakwa, kuuawa, kutekwa na nyumba zao kuchomwa moto.

Mwaka 2017 pekee UNHCR na wadau wake wameripoti visa 12,000 vya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye jimbo la Tanganyika na maeneo ya jirani ya Pweto yaliyoko jimbo la Katanga Juu.

Andrej Mahecic ni msemaji wa UNHCR, Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“UNHCR inatoa tiwo kwa mamlaka za DR Congo zihakikishe ulinzi wa raia na kufuatilia kwa makini ripoti za uhalifu uliofanywa na jeshi na vikundi vilivyojihami na kuachana na fikra ya ukwepaji sheria kwa wakiukaji wa haki.”


Pamoja na wito wa kutaka haki itendeke, Bwana Mahecic amerejelea wito wa UNHCR wa ombi la zaidi ya dola milioni 368 kwa mwaka huu wa 2018 ili kushughulikia janga la kibinadamu linalokumba DR Congo.