Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatujawasahau wana CAR- Mueller

Mtoto nchini CAR apimwa katika juhudi za kuthibiti utapiamlo. Picha: UNICEF

Hatujawasahau wana CAR- Mueller

Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Ursulla Mueller, anaendelea na ziara yake ya siku nne huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Katika siku yake ya pili ya ziara hiyo hii leo amekuwa na mazungumzo na viongozi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu ikiwemo lile la madaktari wasio na mipaka, MSF kwenye mji mkuu, Bangui.

Bi. Mueller amepongeza uwepo thabiti wa MSF nchini humo akitaja miradi 12 ambayo shirika hilo inatekeleza katika majimbo 10 ya CAR.

Amesema miradi hiyo inasaidia kutoa huduma za afya na kwamba katika wiki sita tangu kuanzishwa kwa miradi mipya ya kudhibiti na kusaidia wananchi waliokumbwa na ukatili wa kingono, zaidi ya visa 100 vimeshughulikiwa.

Naibu Mkuu huyo wa OCHA amekuwa pia na mazungumzo na watendajiwa ofisi yake mjini Bangui na kupongeza vile ambavyo wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Na kwa wananchi wa CAR, Bi. Mueller amewahakikishia kuwa..

(Sauti ya Ursulla Mueller)

“Ziara hii kwangu mimi ni fursa ya kujadili masuala ya ulinzi na pia usaidizi wa kibinadamu na pande husika na pia ni fursa ya kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuhusu hatua za usaidizi wa kibinadamu kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Umoja wa Mataifa haujawasahau wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.”