Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Puntland kwa kukabili ukame- de Clercq

Peter de Clercq ambaye ni Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akisalimiana na wakazi wa kijiji cha Salaxley kwenye jimbo la Puntland, nchini Somalia
UN /Ilyas Ahmed
Peter de Clercq ambaye ni Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akisalimiana na wakazi wa kijiji cha Salaxley kwenye jimbo la Puntland, nchini Somalia

Heko Puntland kwa kukabili ukame- de Clercq

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Somalia, katika jimbo la Puntland, harakati za kujikwamua dhidi ya ukame na njaa zinazidi kutia matumaini  lakini bado hatua zaidi zahitajika ili wananchi wasitumbukie tena kwenye baa la njaa.

Mratibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Somalia, Peter de Clercq amepongeza hatua za kukabiliana na ukame sambamba na kuwezesha wananchi kujikwamua na maisha katika jimbo la Puntland, kaskazini mwa nchi hiyo.

Bwana de Clercq amesema hayo leo kwenye mji mkuu wa Puntland, Garowe baada ya kufanya ziara na kuwa na mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Rais wa jimbo hilo Abdilwali Mohamed Ali.

Hata hivyo ameonya kuwa licha ya mafanikio hayo yaliyobainika baada ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Puntland kutathmini hali halisi na kulinganisha hali ilivyokuwa mwaka jana, bado janga la kibinadamu halijamalizika.

Kwa mantiki hiyo Bwana de Clercq ambaye ni Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, amesema wamejadili changamoto zilizosalia kwa sababu bado hali haijatengamaa.

Ametolea mfano maeneo ya Sool na Sanaag akisema bado kuna mahitaji makubwa na uwezekano mkubwa wa kurejea upya kwa mazingira ya njaa.

Hivyo amesema wamejadili jinsi gani ya kuwafikia vyema wakazi wa maeneo hayo kwa kuwapatia misaada ambayo itawawezesha kuepukana na madhara ya ukame na hatimaye njaa.