Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sikukuu ya wapendanao yaleta nuru kwa Dominica

Mwakilishi wa kudumu wa Dominica kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Loreen Bannis Roberts wakati wa  hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia nchi yake.
UNnewskiswahili/Patrick Newman
Mwakilishi wa kudumu wa Dominica kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Loreen Bannis Roberts wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia nchi yake.

Sikukuu ya wapendanao yaleta nuru kwa Dominica

Maadhimisho ya sikukuu ya wapendanao au valentine kwa mwaka huu yalikuja na sura mpya katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani ambapo kulifanyika burudani maalum yenye lengo la kuchangisha fedha kusaidia nchi ya Dominica iliyokumbwa na kimbunga Maria mwezi Septemba mwaka jana.

Ikiwa imeandaliwa na ushirika wa wanawake wa kiarabu pamoja na  nchi 18 wanachama wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Dominica, burudani ilihusisha muziki na mauzo ya keki za chokoleti.

Ili kufahamu hali ya ujenzi hivi sasa kwenye kisiwa hicho, Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imezungumza na Mwakilishi wa kudumu wa Dominica kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Lareen Bannis-Robert ambaye naye alishiriki hafla hiyo.

Sauti ya Loreen Bannis Roberts

 “Hivi sasa tupo katika hatua ya ujenzi upya wa miundombinu, kama unavyojua watu wetu ni wavumilivu sana baada ya janga hilo. Tunashukuru kwa msaada wa nchi mbalimbali, mashirika ya misaada ya jamii ya kimataifa.  Kwa sasa tumetoa kipaumbele katika ujenzi wa nyumba ili watu wetu wapate makazi.” 

Na kuhusu mabadiliko katika ujenzi wa nyumba za kisasa ili kukabiliana na uharibifu wa miundombinu Balozi Lareen amesema..

Sauti ya Loreen Bannis Roberts

“Idara ya ujenzi imewasilishwa maombi kwa serikali kuhusu vifaa vya ujenzi na pia michoro itakayoendana na mazingira yetu. Na wananchi tayari wameanza kuelimishwa kuhusu maeneo ambayo yanafaa kujenga ili kuepuka mafaa. Kama unavyojua Dominica ina mito zaidi ya 300 na watu walijenga hovyo matokeo yake wengi walipoteza maisha.”

Burudani hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa Mataifa na nchi wanachama katika ukumbi wa burudani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa New york.