Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia 10,000 wameuawa Afghanistan 2017-UN

Baada ya mlipuko katikati ya mji mkuu wa Afghanistan Kabul
UNAMA/Jawad Jalali (file)
Baada ya mlipuko katikati ya mji mkuu wa Afghanistan Kabul

Raia 10,000 wameuawa Afghanistan 2017-UN

Amani na Usalama

Nchini Afghanistan raia zaidi ya 10,000 wameuawa au kujeruhiwa mnamo mwaka wa 2017. 

Hii ni kwa mujibu wa  ripoti mpya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikiorodhesha athari za mgogoro wa kivita kwa  raia nchini humo.

Ripoti inaonyesha kuwa raia waliouawa walikuwa 3,438 ilhali waliojeruhiwa ni 7,015 hii ikijumulisha raia wote walioathirika ni 10,453.

Licha ya kwamba idadi hii inaonyesha kupungua kwa asilimia  9 , ikilinganishwa na  mwaka wa 2016, ripoti hii inamulika  idadi kubwa ya majeruhi na mashambulizi ya kujilipua kwa kujitoa mhanga na mashambulio mengine na vilipuzi vya kujitengenezea-IEDs.

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na mkuu wa UNAMA, Tadamichi Yamamoto amesema takwimu pekee haziwezi kuonyesha kikamilifu hali mbaya ya mateso kwa raia wa kawaida.

Aidha ameonyesha wasiwasi wake kuhusu kuendelea kuuumizwa kwa raia wa kawaida kupitia mashambulio ya kujitoa mhanga.

Chanzo cha pili cha madhila kwa raia wa kawaida ripoti inasema ni  mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapinzani.