Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Safari bado ndefu usawa wa kijinsia 2030- Ripoti

Usawa wa kijinsia(maktaba 2016) Planet 50-50
Photo: UN Women/Ryan Brown
Usawa wa kijinsia(maktaba 2016) Planet 50-50

Safari bado ndefu usawa wa kijinsia 2030- Ripoti

Haki za binadamu

Ripoti mpya kuhusu usawa kijinsia katika kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu, SDGs ifikapo mwaka 2030, imebaini kuwa bado kuna safari ndefu kufikia usawa wa kijinsia katika kipindi hicho.

Akizindua ripoti hiyo jijini New York Marekani hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN-Women Phumzile Mlambo Ngucka amesema hata kule ambako kuna matumaini bado utekelezaji wa malengo mengi haufikii wanawake na watoto wa kike.

(Sauti ya Phumzile Mlambo-Ngucka)

 “Mfano mmoja unaoshtua kwenye ripoti hiyo ni kwamba inaonyesha ni kwa jinsi gani bado tuko nyuma kutokomeza vifo vya wajawazito katika nchi maskini na tajiri, ilhali tayari tuna teknolojia na utaalamu wa kuhakikisha uzazi salama na wanawake na watoto wao wanapata huduma muhimu za tiba. Zaidi ya wanawake 300,000 wasingalipaswa kuendelea kufariki dunia kila mwaka kwa sababu ya uzazi.”

Amesema ili kuondoa tatizo hilo ni lazima kuongeza mara tatu juhudi zinazofanyika sasa.

Kuhusu suala la maendeleo kuoanishwa na mafanikio ya usawa wa kijinsia katika kutekeleza SDGs, Bi. Ngucka amesema..

(Sauti ya Phumzile Mlambo-Ngucka)

“Maendeleo, inaonyesha ripoti kuwa si lazima ni hakikisho la maendeleo. Mathalani kiwango cha umaskini kwa kaya zinazoongozwa na mwanamke ni kikubwa kwa nchi kama vile Marekani, Luxembourg, Hispania, Afrika Kusini nchi yangu una Brazil.”

Mapendekezo ni pamoja na kuhakikisha suala la usawa wa kijinsia linajumuishwa katika utekelezaji wa malengo yote 17 kwa kuwa ni mtambuka na zaidi ya yote amesema..

(Sauti ya Phumzile Mlambo-Ngucka)

“Tunahitaji kuondoa pengo la ukosefu wa fedha kwa kuwa katika nchi zote hoja ya wanawake haitengewi fedha za kutosha. Kama ninavyosema wakati mwingine ajenda ya wanawake ina ukata.”

Ripoti hii ya leo ni ya kwanza kuandaliwa na UN-Women tangu kupitishwa kwa SDGs mwaka 2015.