Myanmar shughulikieni tatizo la utaifa kutatua zahma ya Rohingya: UN

13 Februari 2018

Suala la kutokuwa na utaifa ni lazima lishughulikiwe katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ili kutatua zahma ya watu wa Rohingya.

Hayo yamesemwa leo kwenye baraza la usalama na msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu masuala ya kisiasa Miroslav Jenča, alipokuwa akitoa taarifa kwa mabalozi kuhusu machafuko ambayo yamewafungisha virago watu karibu 700,000 kutoka jamii ya walio wachache wa Rohingya na kuvuka mpaka kuingia Bangladesh kusaka usalama tangu mwezi Agost mwaka jana.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na tume ya ushauri iliyopewa jukumu la kuboresha maisha ya watu wote kwenye jimbo la Rakhine lililoko Magharibi mwa Myanmar.

Tume hiyo inayongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, imetoa ripoti mwezi Agosti ambayo inajumuisha mapendekezo yanayojikita katika masuala kama uthibitishwaji wa uraia, haki na usawa mbele ya sheria na uhuru kwa kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Bwana Jenča ameongeza

(SAUTI YA MIROSLAV JENCA)

“Kama ilivyopendekezwa na ripoti ya mwisho ya tume ya ushauri ya Rakhine , tunaitaka serikali kuchukua  jukumu la uongozi katika kuchagiza utangamano katika jamii , kuweka mazingira bora ya majadiliano, kudumisha utamaduni wa kuvumiliana na kuheshimu haki za binadamu baina ya Rakhine na jamii za Rohingya na pia kuharakisha na kutekeleza mchakato wa uthibitishaji uraia  kwa kuzingatia mikataba na viwango vya kimataifa. Kwa jumla kushughulikia vyanzo vyote ni muhimu sana ili kuhakikisha suluhu ya kweli na ya kudumu ya mgogoro huu. Mara zote tumekuwa tukisema tatizo ni kutokuwa na utaifa , hili lazima lishughulikiwe.”

Naye kamishina mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi akizungumza kwenye mkutano huo kwa njia ya video kutoka geneva Uswis amesisitiza kuwa  mazingira bado si shwari kwa wakimbizi hao wa Rohingya kuanza kurejea nyumbani Myanmar kwa hiyari kwani sababu zilizowafungisha virago bado hazijapatiwa suluhu na msaada wa kimataifa unahitajika hasa sasa kuliko wakati mwingine wowote

(SAUTI YA FILIPPO GRANDI)

“Hivi sasa tunakimbizana na muda, wakati zahama kubwa mpya ikijongea, msimu wa Monsoon utakaoanza mwezi Machi. Tumekadiria kwamba zaidi ya wakimbizi 100,000 wanaishi katika maeneo ambayo yako hatarini kwa mafuriko na maporomoko ya udogo. Maelfu kwa maelfu ya watu hususani wakimbizi wasiojiweza wahnahitaji kuhamishwa haraka, maisha yao ko kwenye hatari kubwa.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter