Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si shwari Ituri, DRC, raia waweka maisha yao rehani

Wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwasili kwenye kituo cha  muda cha mapokezi huko Sebagoro, wilaya ya Hoima nchini Uganda
UNHCR/Michele Sibiloni
Wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwasili kwenye kituo cha muda cha mapokezi huko Sebagoro, wilaya ya Hoima nchini Uganda

Hali si shwari Ituri, DRC, raia waweka maisha yao rehani

Amani na Usalama

Amkani si shwari tena kwenye jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako raia wanakimbia mapigano kati ya jamii ya wahemba na walendu. Safari sasa ni kuelekea Uganda kupitia ziwa Albert.

Raia wanaokimbia mapigano ya  kikabila kwenye jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wameelezea madhila wanayokumbana nayo baada ya safari ndefu na ya  hatari ya kuingia Uganda kupitia ziwa Albert.

Mtumbwi ukitia nanga kwenye ufukwe wa ziwa Albert, kila mkimbizi na kirago chake anachoona ni muhimu hapa ugenini, wilaya ya Hoima, nchini Uganda.

Ingawa wamefika salama hapa, wakimbizi hawa wanaweka rehani maisha yao wakikimbia mapigano ya kikabila kwenye jimbo la Ituri nchini DR Congo.

Simulizi za walikotoka ni mbaya ikiwemo wengine kuuawa, na vijiji kuchomwa moto.

Lakini Anita Mave ambaye aliponea chupuchupu anasimulia alichoshuhudia..

(Sauti ya Ana Mave)

Walioponea uhai wao baadhi yao wamebakwa au kutekwa nyara..

Na ndio maana kasi ya kukimbia ni kubwa na sasa wengine wanasubiri chombo kiwasili waweze kuvuka Ziwa Albert na kuingia Uganda miongoni mwano ni Jack Bandinga.

(Sauti ya Jack Bandinga)

Kwa upande wa Uganda, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema msaada zaidi unahitajika kwa wakimbizi kwani chini ya mwezi mmoja wakimbizi zaidi ya 22,000 kutoka DR Congo wamevuka na kuingia Uganda na tayari wanne wamekufa maji ziwani.