Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto 5,000 waliotumikishwa vitani waachiliwa mwaka 2017

Mvulana wa umri wa miaka 15, zamani askari-mtoto akielekea shuleni Sudan Kusini.
UNICEF/Ohanesian
Mvulana wa umri wa miaka 15, zamani askari-mtoto akielekea shuleni Sudan Kusini.

Zaidi ya watoto 5,000 waliotumikishwa vitani waachiliwa mwaka 2017

Amani na Usalama

Wakati leo ikiadhimishwa siku ya kimataifa ya kupiga marufuku watoto kutumikishwa vitani au kuingizwa jeshini, migogoro na ukatili wa vita vimesontwa vidole kwa zahma hiyo.

 

Ikiwa leo Februari 12 kila mwaka huwa siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya watoto vitani, Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo, Virginia Gamba, amesema ongezeko la migogoro na ukatili wa vita  umesababisha watoto kutumikishwa kirahisi kwenye mizozo.

Amesema maelfu ya watoto wakiwemo wavulana kwa wasichana  wanahusishwa katika jeshi pamoja na makundi yenye silaha katika migogoro katika mataifa zaidi ya 20 kote duniani.

Hata hivyo amepongeza azma ya kimataifa ya kumaliza kitendo hicho ambapo kwa mujibuwa takwimu mpya za Umoja wa Mataifa, mwaka 2017 watoto zaidi ya 5,000 waliachiliwa huru na makundi hayo na kujumuishwa kwenye jamii.

Pamoja na kuachiliwa huru, watoto hao bado wanajikuta katika hali ngumu ya mchakato wa kuwarejesha katika jamii zao, hatua moja muhimu ya maisha yao ambayo pia inachangia mwisho wa mzunguko wa ghasia.

(SAUTI YA VIRGINIA GAMBA )

"Jumuiya ya kimataifa inapiga debe sana la kutaka watoto hao waachilie lakini mwisho wa siku fedha ambazo zipo kwa ajili ya ujumuishwaji kwenye jamii wa mtoto hazizidi dola 1500 zinazotakiwa kudumu kwa miezi sita huu sio ujumuishwaji tumekuwa na visa vingi ambavyo hata kiasi hicho hakikuweza kupatikana na watoto waliachwa bila matumaini.

Maadhimisho ya mwaka huu ya siku hii ya kupinga utumikishajiwa watoto yanafanyika ikiwa ni miaka 18 ya itifaki ya haki za mtoto kutotumiwa katika migogoro ya kijeshi.

Itifaki hiyo inaweka umri wa chini wa mtu kusajiliwa katika jeshi katika maeneo ya migogoro kuwa miaka 18 na ilitiwa sahihi na mataifa 167.

Kwa mantiki hiyo Bi. Gamba ameomba kuendelea kuunga mkono  juhudi za pamoja ili mataifa yote duniani yatie saini itifaki hiyo.