Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda yachunguza madai ya rushwa kwenye makazi ya wakimbizi

kamishina mkuu wa UNHCR Filipo Grandi akiwasikiliza wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakati wa ziara yake nchini Uganda .

Uganda yachunguza madai ya rushwa kwenye makazi ya wakimbizi

Serikali ya Uganda inachunguza madai kuwa maafisa wake wanahusika na ufisadi wakati wakiwagawia wakimbizi msaada.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR imepongeza hatua hiyo ya uchunguzi ambao umeamriwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ruhakana Rugunda.

Miongoni mwa madai ni kuwa maafisa hao wanaghushi nyaraka za mgao wa chakula kwa wakimbzi pamoja na kudai hongo kutoka kwa wakimbizi ili wawapatie huduma mbalimbali ilhali huduma hizo  ni za bure.

Mkuu wa ofisi ya kanda ya Afrika ya UNHCR,Valentin Tapsoba, amenukuliwa akisema kuwa shirika lake huchukulia  kwa makaini madai ya ufisadi, udanganyifu na uongozi mbaya, akiongeza kuwa visa vya udanganyifu na vikifanywa na wanaowahudumia wakimbizi husababisha machungu kwa wale wanaowasaidia wenye shida na huondoa imani miongoni mwa wahisani.

Pia amesema kuwa visa hivyo vinapaka matope sera nzuri za kuigwa za Uganda ambayo ni mwenyeji wakimbizi zaidi ya milioni moja.

Sera ya Uganda inakaribisha mkimbizi yeyote na huwapatia haki sawa  kama  raia huku wakipata pia huduma za jamii na ardhi kwa minajili ya kujenga makazi na kulima.