Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ya Sudan Kusini bado ni mtihani mgumu: Soumaré

Mkimbizi wa ndani Sudan Kusini akiwa na mjukuu wake bila kufahamu mustakhbali wa maisha yao kutokana na mzozo nchini mwao tangu mwezi Disemba mwaka 2013.

Amani ya Sudan Kusini bado ni mtihani mgumu: Soumaré

Amani na Usalama

Amani ya kudumu Sudan Kusini bado ni mtihani mgumu unaohitaji juhudi za jumuiya ya kimataifa, serikali ya Sudan, pande zote kinzani nchini humo na mshikamano wa raia wote wa Sudan Kusini.

Hayo yamesemwa na Moustapha Soumaré naibu mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza leo mjini Addis Ababa Ethiopia, kwenye mkutano wa kuhusu Sudan Kusini kwenye baraza la amani na usalama la Muungano wa Afrika, kwa niaba ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS.

Amesema ingawa pande husika katika mzozo wa taifa hilo changa zimeanza kutia matumaini ya mchakato wa kufufua muafaka utakaoleta amani ya kudumu nchini Sudan Kusini bado kuna changamoto kubwa za kibinadamu, kiusalama na kisiasa.

Kwa mwaka huu wa 2018 inakadiriwa watu milioni 7 ikiwa ni zaidi ya mtu mmoja kati ya wawili nchi nzima wanatarajiwa kuhitaji msaada wa kibinadamu, huku mtu mmoja kati ya watatu ambao ni jumla ya watu milioni 4.4 wametawanywa na machafuko na kati yao milioni 1.9 ni wakimbizi wa ndani.

Mkimbizi wa ndani Sudan Kusini akiwa na virago vyake kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo. UNMISS (Maktaba)
UNMISS (Maktaba)
Mkimbizi wa ndani Sudan Kusini akiwa na virago vyake kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo. UNMISS (Maktaba)

Ameongeza kuwa raia wengine takribani milioni 2.4 ni wakimbizi katika nchi 6 jirani. Kwa upande wa uhakika wa chakula bwana Soumaré amesema hii ni zahma nyingine kwani watu karibu milioni tano hawana uhakika wa chakula na msimu wa muambo ukijongea watu 400,000 maisha yao yako hatarini na kusisitiza kuwa ni lazima kuwe na suluhu mbadala ili kuepusha zahma kubwa ya kibinadamu.

Kwa hivyo ameongeza UNMISS, Umoja wa mataifa na mashirika yake  wanajaribu kusaka fursa za kuepusha janga hilo.

Kuhusu usalama , naibu mwakilishi huyo ameelezea mzunguko wa machafuko unaondelea katika baadhi ya sehemu zikiwemo ziwa Warrap, Jonglei, jimbo la Unity na Equatoria Mashariki, hali ambayo amesema ni kumbusho la haja ya kuendelea na mchakato wa amani kwa pande zote husika na pia kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

Amehimiza kuwa suluhu pekee ya machafuko Sudan Kusini ni ya kisiasa na ni utashi kwa pande zote kinzani kuhakikisha kuwa mkataba wa amani unaheshimiwa na unatekelezwa.