Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka ngariba hadi mkunga

Elimu ya kuhamasisha watoto na jamii kuhusu athari za ukeketaji. (Picha:© UNICEF/UNI144402/Asselin)

Kutoka ngariba hadi mkunga

Nchini Djibouti, ngariba aliyekuwa akitumia mikono yake kukeketa watoto wa kike na wanawake, FGM sasa anatumia mikono hiyo kusaidia wanawake wajifungue salama. Ngariba huyo Fatouma Ali baada ya kubadilika amesaidia kuepusha watoto wa kike zaidi ya 200 wasikumbwa na ukeketaji. 

Mjini Djibouti, kwenye mji mkuu wa Djibouti, pembe ya Afrika watoto wa kike wakionekana na bashasha katika nchi ambayo mwaka 1991 asilimia 98 ya wanawake na wasichana walikuwa wenye umri wa kati ya miaka 19 na 49 walikuwa wamekeketwa.  

Huyu ni Fatouma Ali , akisema ughariba ulikuwa ndio kazi yake rasmi..

“Nilifanya ukeketaji kwa mikono yangu mwenyewe. Nilikeketa sehemu ya siri na kwangu mimi pesa ilikuwa kipaumbele. Katu sikufahamu kuwa nilikiuka haki za binadamu. Zamani mtoto wa Kike kama hajakeketwa ilikuwa ni aibu kwa kabila letu.”

Hata hivyo baada ya uhamasishaji na hata viongozi wa dini ya kiislamu kueleza bayana kuwa dini hiyo haitetei ukeketaji au FGM sasa Fatouma anajutia vitendo vya zamani na kuomba msamaha kwa Mungu na zaidi ya yote anasema..

"Sasa mikono hii nimejifunza kuwa mkunga na nasaidia kuzalisha watoto wakiwa hai na wenye afya na furaha “