Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Titov kuongoza uchunguzi wa mauaji ya walinda amani wa TZ

Eneo la Semuliki, huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako walinda amani 15 wa Tanzania waliuawa baada ya kambi yao kushambuliwa tarehe 7 disemba 2017. Hadi leo mlinda amani mmoja hajulikani aliko. (Picha:UNPeacekeeping)

Titov kuongoza uchunguzi wa mauaji ya walinda amani wa TZ

Dmitry Titov kutoka Urusi ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuongoza uchunguzi maalum wa mashambulio huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, yaliyosababisha vifo vya walinda amani 15 wa Tanzania na wengine 43 walijeruhiwa huku mmoja hajulikani alipo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa jopo hilo maalum litachunguza mazingira kuhusiana na tukio hilo la tarehe 7 mwezi uliopita huko Semuliki jimbo la Kivu Kaskazini.

Halikadhalika litatathmini utayari wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko DRC, MONUSCO na hatua zilizochukuliwa siku hiyo.

Jopo hilo ambalo litakuwa pia na maafisa wawili wa jeshi kutoka Tanzania, litapendekeza jinsi ya kuzuia mashambulizi kama hayo siku zijazo na iwapo yatatokea yasiwe na madhara makubwa.

Katika kufanya uchunguzi huo, Bwana Dmitrov na jopo lake watakwenda DRC mapema mwezi huu na maeneo mengine ya ukanda wa Maziwa Makuu.

Bwana Titov alijiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 1991 ambapo ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwemo msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu utawala wa sheria na mkurugenzi wa  kitengo cha Afrika kwenye idara ya ulinzi wa amani.