Maandamano Iran hayajaathiri sana shughuli za UN

5 Januari 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mkutano wa wazi kuhusu hali inayoendelea nchini Iran, kufuatia maandamano yaliyofanyika nchini humo tangu tarehe 28 mwezi uliopita hadi Jumanne wiki hii.

Akiwasilisha ripoto kuhusu kilichotokea na hali ya sasa, Naibu Mkuu wa Idara ya masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Tayé-Brook Zerihoun amenukuu vyombo vya habari vilivyoonyesha msingi wa maandamano hayo kuwa ni waandamanaji kuchukizwa na mpango wa serikali wa kupunguza matumizi ya kijamii huku pesa zaidi ikielekezwa kwenye mipango ya kijeshi na kidini.

Hata hivyo amesema..

(Sauti ya Tayé-Brook Zerihoun)

“Hadi hii leo, shughuli za maendeleo za Umoja wa Mataifa nchini Iran hazijaathiriwa na matukio ya hivi karibuni. Sekretarieti itaendelea kufuatilia hali ilivyo nchini humo na kushirikisha mamlaka za Iran kwa lengo la kuchangia kwenye jitihada kama alivyoeleza Katibu Mkuu tarehe 3 Januari, kushughulikia shaka halali za wananchi kwa njia ya amani na kuepusha ghasia au visasi dhidi ya wanaoandamana kwa amani.”

Katika mkutano huo, Marekani kupitia mwakilishi wake wa kudumu, Nikki Haley imetaka jamii ya kimataifa kutofumbia macho kinachoendelea Iran na kuchukua hatua.

Naye mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Matthew Rowcroft ametoa wito kwa Iran kuzingatia haki ya raia wake kuandamana kwa amani.

Kwa upande wao Urusi na China kupitia wawakilishi wao kwenye Umoja wa Mataifa wamesema suala la Iran ni suala la ndani ya nchi kwa hiyo Baraza la Usalama halipaswi kuingilia na badala yake lijikite kwenye masuala yanayoendana na mamlaka yake.

Naye mwakilishi wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Gholamali Khoshroo amesema hatua ya Baraza la Usalama kukubali kuitisha kikao cha leo ni kinyume siyo tu na makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, JCPOA bali pia ni kinyume na misingi ya baraza hilo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter