Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila Afrika, hatutasonga mbele- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (Kushoto) akiwa na Moussa Faki, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU baada ya kutia saini mfumo wa ushirikiano kati ya vyombo hivyo viwili. (Picha: UN/Antonio Fiorente)

Bila Afrika, hatutasonga mbele- Guterres

Umoja wa Mataifa umesema ushirikiano kati yake na Muungano wa Afrika, AU, ni jambo la msingi ili umoja huo uweze kutekeleza majukumu yake.

Hayo yamesemwa hii leo huko Addis Ababa, Ethiopia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres baada ya kutia saini mpango wa ushirikiano kati ya vyombo hivyo viwili.

Miongoni mwa majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kusimamia na kulinda amani duniani ambapo Bwana Guterres amesema anaamini kwamba katika masuala ya amani, ulinzi, maendeleo na haki za binadamu, bara la Afrika ndio ufunguo wa suluhu ya matatizo yanayokumba dunia hivi sasa.

Ametolea mfano suala la wakimbizi ambalo sasa ni changamoto kubwa duniani akisema  Afrika licha ya changamoto zake, zimefungua milango kwa ajili ya wakimbizi  na wahamiaji.

Kuhusu maendeleo Bwana Guterres amesema jamii ya kimataifa katu haitaweza kufanikiwa kimaendeleo iwapo Afrika haitaweza kunufaika kimaendeleo kutokana na idadi kubwa ya vijana iliyopo hivi sasa barani huo na pia kushughulikia mizozo inayoendelea.

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa uko bega kwa bega na Afrika huku ikiheshimu uongozi wa chombo hicho katika kusaka suluhu ya matatizo na kusonga katika mwekeleo bora.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa yuko nchini Ethiopia kushiriki vikao vya mkutano wa viongozi wa Muungano wa Afrika ambapo pia ameshiriki kikao cha kutathmini ubia wa kutokomeza njaa Afrika.

Bwana Guterres amewaeleza viongozi hao kuwa matumaini ya awali ya kutokomeza njaa barani  humo yamefifishwa kutokana na mizozo na mabadiliko ya tabianchi.

Kama hiyo haitoshi mfumo wa soko ni dhaifu, halikdhalika miundombinu.

Kwa mantiki hiyo amesema serikali zinapaswa kuweka mazingira ambamo kwayo sekta binafsi itawekeza na hivyo kunufaisha siyo tu maskini bali pia kuhakikisha kuna chakula cha kutosha.