Utapia mlo wawazonga watoto Venezuela:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la UNICEF limeonya kuwa idadi kubwa ya watoto nchini Venezuela wanakabiliwa utapiamlo kutokana na athari za mgogoro wa kiuchumi unaolikumba taifa hilo.
Ingawa takwimu kamili hazipo kutokana na kutopatikana kwa data za lishe na za afya , kuna dalili tosha za kuwa mgororo huo unawazuia watoto kupata huduma bora za afya, madawa pamoja na lishe.
Hali hiyo imelilazimisha shirika la UNICEF kutoa wito wa kutekeleza mkakati wa dharura wa kukabiliana na utapiamlo kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wake.
Takwimu rasmi na pekee zilizoko ni za mwaka 2009 ambazo zinaonyesha afya duni kutokana na ulinganifu wa uzito na urefu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, wakati huo ulikuwa asili mia 3.2. Hata hivyo takwimu mpya na ambazo si rasmi, zimeonyesha kama idadi ya watoto wenye afya duni ni kubwa zaidi.
Nayo ripoti ya dunia ya lishe ya mwaka 2016 inakadiria kwamba kiwango cha afya duni miongoni mwa watoto ni asilimia 4.1 huku ripoti ya taifa kuhusu chakula na lishe duniani ya mwaka 2017 ikisema kwamba kiwango cha lishe duni nchini Venezuela kimeongezeka.