Umoja wa Mataifa walaani vikali vifo vya makusudi vya wahamiaji 30

26 Januari 2018

Mashirika ya Umoja wa Mataifa , la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la uhamiaji IOM leo wamelaani vikali na kuelezea simanzi yao baada ya kuthibitisha vifo vya wahamiaji 30 waliozamishwa maksidi pwani ya Yemen wiki hii. Tupate taarifa Zaidi na Selina Jerobon.

(TAARIFA YA SELINA JEROBON)

Kwa mujibu wa mashirika hayo,  watu hao walifariki Dunia  baada ya boti yao iliojaa pomoni kuzama. Boti hiyo inayomilikiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu ilikuwa imebeba  wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanarejea Pembe ya Afrika wakitoroka machafuko nchini Yemen.

Msemaji wa  IOM, Joel Milliman, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuwa IOM na shirika la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR wameshtushwa na kusikitishwa na tukio hilo la kuzama kwa takriban wakimbizi 30 kwenye mwambao wa Aden, Yemen, kisa kilichotokea mapema wiki hii na kuthibitishwa leo.

Manusra  wanasema boti hiyo iliyokuwa ikielekea Djibouti ilifurika kupita kiasi,ikiwa na jumla ya wahamiaji  152 raia wa Somalia 51 na wa  Ethiopia 101 na kuongeza

(SAUTI YA JOEL MILMAN)

“Chombo hicho, inaaminiwa kilikuwa kinasimamiwa na wasafirishaji haramu waliokuwa wanajaribu kuwasafirisha wakimbizi na wahamiaji hadi Djibouti huku wakiomba pesa kutoka kwa wakimbizi hao pamoja na wahamiaji kwa nguvu. Inasemekana kuwa chombo hicho kilizama kukiwa na taarifa za ufyatuaji risasi dhidi ya abiria hao.”

IOM na washirika wake wamekuwa wakitoa msaada wa dharura kama vile madawa,chakula maji kwa manusura.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter