Ni wakati wa kubadili taswira ya mgogoro wa Mashariki ya Kati: Mladenov

25 Januari 2018

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nicolay Mladenov amesema ni muhimu kujenga mazingira ya kuanza upya mazungumzo ya amani kati ya pande mbili kinzani za Israel na Palestina kwani suluhu pekee ya amani ya kundumu katika eneo hilo ni mazungumzo.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nicolay Mladenov amesema ni muhimu kujenga mazingira ya kuanza upya mazungumzo ya amani kati ya pande mbili kinzani za Israel na Palestina kwani suluhu pekee ya amani ya kundumu katika eneo hilo ni mazungumzo.

Mladenov amesema hayo leo akihutumbia kikao cha baraza la usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati kwa njia ya video kutokea mjini Yerusalemu na kuongeza

(SAUTI YA NIKOLAY MLADENOV1)

“Hatuwezi kusubiri zaidi kubadili hali mbaya ya sasa katika mgogoro huu. Kila ujenzi wa makazi ya kinyume cha sheria, kila mtu aliyeuawa na kila juhudi zilizoshindwa Gaza, zinafanya kuwa vigumu zaidi kwa Wapalestina na Israel kumaliza tofauti zao, kujenga imani na kuwekeza katika lengo la kutatua migogoro. Ni wakati wa kumaliza kasumba hii ya uharibifu na kuanza tena kuweka msingi wa amani.”

image
Hali ilivyokuwa kwenye nyumba ya mmoja wa wapalestina baada ya kubomolewa na mamlaka ya Israeli. (Picha:Unifeed/Video capture)

Ameongeza kuwa baada ya miaka 25 ya mkataba wa Oslo wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati sasa ni wakati wa vitendo badala ya maneno matupu kwa pande zote. Kuhakikisha masuala tete yanapatiwa ufumbuzi ikiwemo ujenzi wa makazi ya Walowezi, kutekeleza makubaliano ya kimataifa na pia kuonyesha uongozi wa kisiasa na kuondoa vikwazo vya kupatikana suluhu ya kudumu kwani(SAUTI YA NIKOLAY MLADENOV2)

"Uchaguzi wetu uko wazi ama tuchukue hatua za haraka za kubadili hali hii ya hatari au tujiweke hatarini kwa zahma nyingine ya kibinadamu.”

Na kuhusu hatua ya Marekani kukata msaada kwa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA amesema

(SAUTI YA MLADENOV3)

"Wakati tunashukuru kwa ahadi ya karibuni ya Marekani ya dola milioni 60, kiasi hiki kinawakilisha punguzo kubwa kuliko mchango wa Marekani wa jadi, na linaongeza wasiwasi kwa jamii ya wakimbizi  wa Palestina milioni 5.3, ambao tayari wameathirika na mgogoro wa muda mrefu wa wakimbizi duniani, ambao ni miaka 70 sasa. "

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter