Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya haki za binadamu DRC mwaka 2017 ilizidi kuwa mbaya

Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakikimbia ghasia jimbo la Ituri. Picha: UM

Hali ya haki za binadamu DRC mwaka 2017 ilizidi kuwa mbaya

Haki za binadamu

Ukiukaji wa haki za binadamu uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 25 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwaka uliopita ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, imesema ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja waMataifa nchini humo hii leo. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Vitendo hivyo ni pamoja na mauaji ya raia kinyume cha sheria, kukamata watu kiholela, ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto pamoja na utumikishaji watoto jeshini.

Sababu kuu ya ongezeko hilo ni pamoja na kubinywa kwa demokrasia na kupanuka kwa maeneo yenye mapigano huku ghasia hizo nazo zikiwa na athari kubwa zaidi.

Ingawa vikundi vilivyojihami vimetajwa kuhusika na vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki kwa asilimia 38, vikosi vya ulinzi na usalama vya DRC navyo vimetajwa kuhusika na ukiukaji wa haki dhidi ya raia.

Abdoul Aziz Thioye ni Naibu Mkuu wa ofisi hiyo ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC.

(Sauti ya Abdoul Aziz Thioye )

“Ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inalaani ongezeko kubwa la idadi ya watu waliokumbwa na visa vya mauaji kiholela, kukamatwa hovyo na kuuaawa kinyume cha sheria. Idadi hiyo ni takribani watu 1,180 ambayo ni ongezeko la aina yake la asilimia 146 kwa mwaka kwa vitendo vilivyofanywa na jeshi na polisi wa serikali.”

Maeneo yaliyotajwa kukumbwa zaidi na ukatili huo ni huko jimbo la Kivu Kaskazini na Kasai kulikoshamiri harakati za kukabiliana na kikundi kilichojihami cha Kamuina Nsapu.